IQNA

Waislamu Warohingya

Mkuu wa Haki UN atembelea kambi ya Wakimbizi Waislamu Warohingya nchini Bangladesh

18:34 - August 14, 2022
Habari ID: 3475618
TEHRAN (IQNA)- Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu Michelle Bachelet amewasili Bangladesh siku ya Jumapili katika safari ya siku nne ambayo inajumuisha kutembelea kambi za wakimbizi zenye hali mbaya ambapo zaidi ya wakimbizi milioni wa Rohingya kutoka Myanmar wanaishi.

Ziara hiyo inakuja miaka mitano baada ya jeshi la Myanmar kufanya mauaji ya halaiki dhidi ya Waislamu walio wachache wa Rohingya nchini humo, na kuwalazimisha watu wa jamii hiyo kuhamia nchi jirani kama vile Bangladesh na India.

Serikali ya Myanmar ya kiongozi mkuu wa zamani Aung San Suu Kyi, ambaye aliondolewa madarakani na jeshi katika mapinduzi, iliunga mkono ukandamizaji wa kijeshi dhidi ya Waislamu wa Rohingya. Hata alisafiri hadi The Hague mnamo Desemba 2019 kutetea ukatili wa jeshi.

Maelfu ya Waislamu wa Rohingya waliuawa, kubakwa, kuteswa, au kutiwa mbaroni na vikosi vya kijeshi, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, ambao umeitaja jamii  hiyo ya Jimbo la Rakhine Magharibi mwa Myanmar kuwa ndio watu wachache wanaonyanyaswa zaidi duniani.

Hivi sasa, takriban wakimbizi 850,000 wa Rohingya wamesalia kukwama katika mazingira duni na msongamano wa watu katika kambi za wakimbizi nchini Bangladesh.

Katika ziara yake hiyo, Bachelet atakutana na Waziri Mkuu wa Bangladesh Sheikh Hasina, ambaye naye ana rekodi ya ukiukaji wa haki za binadamu.

Makundi tisa ikiwa ni pamoja na Human Rights Watch yalisema kwamba Bachelet anapaswa "kutoa wito hadharani kukomesha mara moja unyanyasaji mkubwa ikiwa ni pamoja na mauaji ya kiholela, mateso, na kutoweka kwa nguvu" nchini Bangladesh.

Hata hivyo, Bangladesh inakanusha madai hayo na kusema kwamba itaangazia "juhudi zake za dhati za kulinda na kukuza haki za binadamu za watu."

3480091

Kishikizo: rohingya ، waislamu ، bachelet ، myanmar
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha