IQNA

Waislamu Warohingya

Wito wa kutatua matatizo ya Waislamu Warohingya wanaoteseka

17:21 - August 28, 2022
Habari ID: 3475696
TEHRAN (IQNA)- Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa mwito kwa jamii ya kimataifa kuwasaidia kwa hali na mali wakimbizi Waislamu wa Rohingya walioko nchini Bangladesh.

Noeleen Heyzer alitoa mwito huo Alkhamisi usiku katika siku ya nne ya safari yake ya kuitembelea Bangladesh na kusisitiza kuwa, Wabangladesh wameendelea kuwa wakarimu kwa wakimbizi Warohingya, na kuna haja kwa nchi za dunia na hususan za eneo kuisaidia serikali ya Dhaka kubeba mzigo wa kushughulikia maslahi ya wakimbizi hao.

Ameeleza bayana kuwa, jamii ya kimataifa ina wajibu wa kutafuta suluhu jumuishi, pana na ya kudumu ya mgogoro huo, na kwamba mgogoro huo katu haufai kusahaulika au kupuuzwa.

Hatua ya jeshi la Myanmar ya kuwapokonya uraia Waislamu wa jamii ya Rohingya, kuchoma moto nyumba zao, kufanya mauaji dhidi ya jamii hiyo na vitendo vingine vya kinyama ni mambo ambayo yaliwalazimisha Waislamu hao kuyakimbia makazi yao. Zaidi ya wakimbizi Waislamu milioni moja wapo katika kambi za wakimbizi kwenye eneo la kambi ya Cox’s Bazar nchini Bangladesh.

Wakimbizi hao hawana kabisa huduma za awali za kimsingi kwa ajili ya maisha kama vile afya, tiba na sehemu za malazi. Akthari ya Waislamu jamii ya Rohingwa wanaishi kwa kutangatanga katika mataifa mbalimbali kama India, Malaysia, Indonesia na hata Saudi Arabia.

Licha ya kuwa Umoja wa Mataifa umetuma mara chungu nzima maripota na timu zake kadhaa za wataalamu kwa ajili ya kufanya uchunguzi kuhusiana na hali ya wakimbizi hao Waislamu wa Kirohingya na hata kutolewa ripoti nyingi na tofauti zinazoonyesha kuwa wanakabiliwa na hali mbaya, lakini kivitendo taasisi hiyo kubwa ya kimataifa haijachukua hatua yoyote ya kuyapatia ufumbuzi matatizo ya wakimbizi hao. Si hayo tu bali kadiri siku zinavyosonga mbele ndivyo matatizo ya Waislamu hao yanavyozidi kuwa tete.

Sajjad Rezapour, mweledi wa masuala ya kusini mashariki mwa Asia anasema kuhusiana na hili: Jamii ya kimataifa imepuuza kabisa hali ya Waislamu wa jamii ya Rohingya. Kurefuka muda wa maisha yao ya ukimbizi katika mataifa mbalimbali na kushindwa jamii ya kimataifa kuzilazimisha serikali zilizoingia madarakani nchini Myanmar katika miaka ya hivi karibuni ili ziwapokee Waislamu hao ambao asili yao ni jimbo la Rakhine nchini Myanmar ni jambo ambalo limeifanya jamii ya kimataifa iwasahau wakimbizi hao wanaotaabika.

Katika suala hili, Umoja wa Mataifa una nafasi muhimu mno katika kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Myanmar hasa kwa kuzingatia kuwa, kwa mujibu wa umoja huo, Waislamu wa Rohingya ndio jamii iliyodhulumiwa zaidi miongoni mwa kaumu na jamii za waliowachache.

Umoja wa Mataifa kwa kutumia uwezo mbalimbali ulionao kama Baraza la Usalama unaweza kuchukua hatua muhimu zaidi kwa ajili ya kuhitimisha dhulma na ukandamizaji wa serikali ya Myanmar dhidi ya Waislamu wa Kirohingya. Hasa kwa kutilia maanani kwamba, asili ya Waislamu hao ni Myanmar tangu enzi za mababu zao. Hata hivyo jeshi la Myanmar na mabudha wenye misimamo mikali wakiwa na tamaa ya mali na ardhi za Waislamu Warohingya hususan katika mkoa wa Rakhine, wamekuwa wakiendesha vitendo vya kinyama kama kuchoma moto nyumba na ardhi za Waislamu hao na hivyo kuwafanya walazimike kuwa wakimbizi.

Alaa kulli haal, mkataba uliotiwa saini baina ya serikali ya Bangladesh na Myanmar kabla ya mapinduzi ya kijeshi huko Myanmar ambapo ilikubaliwa kurejea hatua kwa hatua kwa wakimbizi wa Kirohingya, baada ya wanajeshi kuingia madarakani nchini Myanmar si tu kwamba wamebatilisha makubaliano hayo, bali wamelipuuza na kulitupilia mbali kabisa suala la wakimbizi hao. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana wajuzi wa mambo wanaamini kuwa, Umoja wa Mataifa una nafasi muhimu katika kadhia hii kuliko wakati mwingine wowote ule, na ndio maana jamii ya kimataiifa inataraji kuiona taaisis hiyo ikiacha kutosheka tu na kutoa ripoti, bali ichukue hatua za maana na za kivitendo kwa ajili ya kuhitimisha matatizo ya wananchi hao.

4081223

captcha