IQNA

Jinai za Israel

Wafungwa Wapalestina katika jela za Israel waendeleza mgomo wa kula

21:58 - August 25, 2022
Habari ID: 3475679
TEHRAN (IQNA)- Kuanzia 22 Agosti, mateka wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika jela za kuogofya za utawala wa Kizayuni wa Israel walianzisha mgomo usio na kikomo wa kula chakula wakilalamikia hatua za kidhalimu na maafisa wa utawala huo katika magereza.

Bodi ya Wafungwa Wapalestina imesema kuwa, hali ya taharuki imetanda katika jela na magereza ya utawala wa Kizayuni, baada ya mateka hao wa Kipalestina kuanza mgomo wa kula chakula siku ya Jumatatu.

Kamati Kuu ya Dharura ya Wafungwa wa Kipalestina imetangaza kuwa, mgomo huo wa kula ulianza Jumatatu na kundi jingine la wafungwa litaanza leo Jumatano, kabla ya kuzinduliwa katika magereza na jela zote za Wazayuni wanakoshikiliwa kidhulma Wapalestina.

Mgomo huo wa kula ni muendelezo wa hatua za wafungwa wa Kipalestina, ambao wanalalamikia hali mbaya ya kibinadamu katika jela hizo za Wazayuni. Mateka zaidi ya 500 wa Kipalestina wamekataa kwenda kusikiliza kesi dhidi yao katika mahakama za kijeshi za Israel, tokea mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa.

Ripoti zinaonyesha kuwa, kuna wafungwa 4,600 wa Kipalestina katika magereza ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Mateka hao wa Kipalestina wamekuwa wakikabiliwa na vitendo mbalimbali kama vya maudhi na mateso vinavyofanywa na maafisa magereza. Mwenendo wa vitendo hivyo siyo tu kwamba, unaendelea bali umechukua mkondo wa kuongezeka.

Ukweli wa mambo ni kuwa, kila mara kunapoongezeka mzozo, mvutano na mapigano baina ya Wazayuni na Wapalestina mateso dhidi ya Wapalestina katika magereza ya utawala huo ghasibu nayo huongezeka na kushadidi. Ni kama vile maafisa wa Israel humalizia hasira zao kwa wafungwa na mateka wa Kipalestina baada ya kushindwa kukabiliana na wanamapambano wa Palestina. Wafungwa wa Kipalestina daima wamekuwa wakihamishwa kutoka seli moja kwenda nyingine.

Baada ya kushadidi mateso na vitendo visivyo vya kibinadamu, wafungwa wa Kiplaestina waliamua kuanzisha mgomo wa kula chakula kuanzia siku ya Jumatatu kwa shabaha ya kulalamikia vitendo vya kidhalimu vya maafisa magereza katika jela za utawala huo ghasibu na vamizi. Lengo la mgomo huo wa kula ni kuzishinikiza mamlaka za magereza kutekeza makubaliano ili kwa njia hiyo mateka wa Kipalestina wapate haki zao hususan kuboreshewa mazingira ya magereza.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotangazwa ni kuwa, takribani Wapalestina milioni 1 wametipia tajiriba ya kushikiliwa mateka katika magereza ya Israel kuanzia mwaka 1967 hadi sasa. Idadi hii inaundwa asilimia 20 ya taifa la Palestina. Kwa msingi huo, suala la mateka wa Kipalestina ni hasasi na nyeti mno la linaweza kusababisha kutokea mlipuko wa hali ya mambo katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza.

4080730

captcha