IQNA

Hamas yalaani mauaji na mateso ya wafungwa Wapalestina wanaoshikiliwa na Israel

15:23 - November 27, 2025
Habari ID: 3481575
IQNA-Harakati ya Kiislamu ya Kupigania Ukombozi wa Palestina (Hamas) imelaani vikali mauaji ya makusudi na mateso ya Wapalestina walioko katika magereza ya kuogofya ya utawala haramu wa Israel, ikiyataja kama “uhalifu kamili wa kivita” na kuitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua madhubuti.

Katika taarifa yake ya Alhamisi, Hamas imesema kuwa utawala wa Kizayuni umegeuza magereza yake kuwa vituo vya mateso na mauaji ya moja kwa moja dhidi ya wafungwa wa Kipalestina.

Tangu Israel ilipoanzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza mnamo Oktoba 2023, makumi ya wafungwa Wapalestina wameuawa na wengine wengi kuteswa kwa ukatili. Hamas imeripoti kuwa angalau Wapalestina 94 wamefariki wakiwa kizuizini tangu Oktoba 2023, huku mashirika ya haki za binadamu na manusura wakitoa ushahidi wa unyama wa kutisha, ikiwemo kupigwa vibaya, kumwagiwa maji ya moto, kushambuliwa na mbwa, ukatili wa kingono, pamoja na kunyimwa chakula, usingizi na huduma za afya.

Hamas imesema kuwa magereza haya yamegeuzwa kuwa viwanja vya mauaji ya moja kwa moja ili kuangamiza watu wao, na ikasisitiza kuwa vitendo hivyo ni uhalifu wa kivita chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu vinavyofichua asili ya kikatili ya utawala wa Kizayuni. Harakati hiyo imeutaka Umoja wa Mataifa, mashirika ya haki za binadamu, na jumuiya ya kimataifa kuishinikiza Israel kusitisha ukatili huu na kuhakikisha haki za wafungwa zinalindwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Kwa sasa, inakadiriwa kuwa zaidi ya Wapalestina 10,000, wakiwemo wanawake na watoto, wanashikiliwa katika magereza hatari ya Israel.

Aidha, tangu ianzishe vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza Oktoba 2023, Israel imeua takribani Wapalestina 70,000 na kuwajeruhi zaidi ya 170,000 katika eneo hilo ambalo bado liko chini ya mazingiro.

Hujuma za Israel dhidi ya wapiganaji

Wakati huo huo, Hamas imelaani vikali kitendo cha kikatili cha utawala wa Kizayuni cha kuwafuatilia, kuwaua na kuwakamata wapiganaji waliokuwa wamezingirwa ndani ya mitaro ya mji wa Rafah.

Hamas imetaja hatua hiyo kuwa ni uvunjaji wa wazi wa makubaliano ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza, na ikasisitiza kuwa tukio hilo ni ushahidi thabiti wa juhudi za kudumu za utawala huo za kudhoofisha na kuangamiza makubaliano ya amani yaliyopo.

Hamas imesema a kuwa katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita imefanya juhudi kubwa kwa kushirikiana na viongozi wa kisiasa na wapatanishi mbalimbali ili kutatua tatizo la wapiganaji waliokuwa wamezingirwa na kuhakikisha kurejea kwao majumbani mwao. Hamas imeeleza kuwa tayari ilikuwa imewasilisha mawazo na mifumo mahsusi ya kushughulikia suala hilo, na imekuwa katika mawasiliano ya karibu na wapatanishi pamoja na serikali ya Marekani, ambayo ni miongoni mwa wadhamini wa makubaliano ya kusitisha mapigano.

Hamas imeongeza kuwa, licha ya juhudi hizo, utawala wa Kizayuni umevuruga kila hatua kwa kuendeleza mauaji, jinai, ufuatiliaji na ukamataji wa wapiganaji hao. Hatua hiyo, kwa mujibu wa Hamas, ni ishara ya kushindwa kwa juhudi za wapatanishi waliokuwa wakijitahidi kwa nguvu kubwa kushirikiana na pande mbalimbali za kimataifa ili kumaliza mateso ya wapiganaji mashujaa wa Palestina.

4319428

captcha