IQNA

Mgogoro

Mvutano kati ya Morocco na Tunisia kuhusu Sahara Magharibi

11:23 - August 29, 2022
Habari ID: 3475698
TEHRAN (IQNA)- Morocco imemuita nyumbani balozi wake wa Tunisia kulalamikia kitendo cha Rais wa Kais Saied wa Tunisia kumpokea kiongozi wa harakati ya Polisario inayopigania kujitenga eneo la Sahara Magharibi.

Morocco imesisitiza kuwa, hatua ya Tunisia ya kumualika Brahim Ghali, kiongozi wa Harakati ya Uhuru wa Polisario katika mkutano wa maendeleo wa Japan na Afrika unaofanyika jijini Tunis, ni kitendo kiovu kilichowakasirisha Wamorocco.

Tunisia pia imejibu hatua ya Morocco na imetangaza kumuita nyumbani balozi wake wa mjini Rabat kwa ajili ya mashauriano. Viongozi wa nchi kadhaa za Afrika wanashiriki mkutano huo uchumi jijini Tunis wikendi hii.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Tunisia leo Jumamosi imesema katika taarifa kwamba, Tunis itaendelea kuwa na msimamo wa kati juu ya kadhia ya Sahara Magharibi.

Morocco inaliangalia eneo la Sahara Magharibi, ambalo ni koloni la zamani la Uhispania, kuwa ni eneo lililo chini ya mamlaka yake, wakati jirani yake Algeria inaiunga mkono na kuipa hifadhi Harakati ya Polisario inayopigania ukombozi na kujitawala kwa eneo hilo tokea miaka ya 70.

Vita vya kupigania uhuru baina ya harakati ya Polisario na Morocco vilianza mwaka 1975 na  kuendelea hadi mwaka 1991 na kisha pande mbili zilisitisha mapigano kwa upatanishi wa Umoja wa Mataifa.

3480252

captcha