IQNA

Hali ya Tunisia

Ennahda ya Tunisia yailaumu serikali kwa kukiuka haki haki za wapinzani wa kisiasa

23:23 - January 25, 2023
Habari ID: 3476464
TEHRAN (IQNA) - Harakati ya Kiislamu ya Ennahda ya Tunisia ilizitaja hukumu zilizotolewa dhidi ya mkuu wa kambi ya Muungano wa ‘Heshima’, Seifeddine Makhlouf, wakili Mahdi Zaqrouba na wabunge kadhaa wa muungano huo kuwa "zisizo za haki na mfano hatari".

Makhlouf alihukumiwa kifungo cha miezi kumi na nne jela na Zaqrouba miezi kumi na moja kwa kujaribu kusafiri licha ya kuwa na marufuku ya kusafiri.

Katika taarifa kupitia Facebook, Ennahda ilionyesha mshikamano wake na kila mtu aliyeathiriwa na hukumu hizo. "Tunatoa wito wa kuachiliwa kwa washtakiwa, kukomeshwa kufikishwa raia katika mahakama za kijeshi, na kukomeshwa kwa ukandamizaji dhidi ya wapinzani wa mapinduzi ya kiria."

Harakati hiyo ya upinzani ilisema ‘utawala wa mapinduzi ya kiraia" unaoongozwa na  Rais Kais Saied  unabeba dhima ya ukiukaji "wazi " wa haki za wapinzani wa kisiasa.

"Kuwashitaki mbele ya mahakama za kijeshi na kutoa hukumu ambazo zinaanza kutekelezwa  haraka kunakiuka vifungu vya sheria, kwani hawawezi kukata rufaa," ilisema taarifa hiyo.

Mnamo Julai 25, 2021, Rais Kais Saeid, alipitisha maamuzi na kuchukua hatua kadhaa zisizo za kawaida ikiwemo kutangaza kufuta mamlaka ya Bunge, kuondolewa kwa kinga ya Wabunge, kumfuta kazi Waziri Mkuu na kuvunja tume ya usimamizi wa katiba, hatua ambazo zimetajwa kuwani ‘mapinduzi ya kiraia.’

Hatua hizo za Rais Saied zilizusha mtafaruku na mkwamo wa kisiasa nchini Tunisia, ambao uliambatana na wimbi la maandamano ya vyama na mirengo ya kisiasa, kikiwemo chama cha Kiislamu cha Ennahda.

Wapinzani wanasisitiza hatua za Rais wa Tunisia kuwa ni mapinduzi dhidi ya katiba iliyoidhinishwa mwaka 2014 na mabadiliko ya kidemokrasia yaliyopatikana kupitia mapinduzi ya umma ya mwaka 2011 yaliyohitimisha utawala wa kidikteta wa Zine El Abidine Ben Ali, lakini Saied mwenyewe anasisitiza kuwa, hatua zake zimelenga kuiokoa Tunisia na msambaratiko wa kiuchumi na kijamii.

3482205

captcha