IQNA

Harakati ya Kiislamu ya Amal ya Jordan

Mapatano ya Israel na Morocco ni uhaini wa kihistoria

20:37 - December 25, 2020
Habari ID: 3473491
TEHRAN (IQNA) – Harakati ya Kiislamu ya Amal ya Jordan imetoa taarifa na kusema hatua ya Morocco kuafiki kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel ni kashfa kubwa na pia ni uhaini wa kihistoria.

Katika taarifa, Harakati ya Amal ambayo ni tawi la kisiasa la Harakati ya Ikwanul Muslimin nchini Jordan imelaani vikali kitendo cha Morocco kukubali kuanzisha uhusiano na utawala ghasibu wa Israel.

Harakati ya Kiislamu ya Amal ya Jordan imesema mapatano hayo ni pigo kubwa kwa kadhia ya Palestina , harakati za muqawama na mapambano ya Kiislamu.  Aida harakati hiyo imesema kuanzisha uhusiano na Israel ni uhani kwa misimamo ya mataifa ya eneo ambayo yanapinga uanzishwaji uhusiano wa kawaida na utawala bandia wa Israel ambao ni adui nambari moja wa Ulimwengu wa Kiislamu.

Harakati ya Kiislamu ya Amal ya Jordan imetoa wito kwa watu wa Morocco na vyama huru vya kisiasa nchini humo kuchukua hatua za dharura kukabiliana na mpango mchafu wa uanzishwaji uhusiano baina ya nchi yao na Israel.

Mapema mwezi huu wa Disemba, Mfalme wa Morocco Mohammed VI alimwarifu Rais Donald Trump wa Marekani kwenye mazungumzo kwa njia ya simu kuwa amekubali kurejesha mawasiliano ya kiserikali na kuanzisha uhusiano wa kibalozi na utawala wa Israel haraka iwezekanavyo.

Marekani nayo ilisema itatambua mamlaka ya Morocco katika eneo la Sahara Magharibi la nchi hiyo ambalo limejitangazia uhuru. Ufalme wa Morocco umetangaza kuwa Marekani hivi karibuni itafungua ubalozi mdogo huko Sahara Magharibi.

Uamuzi huo wa Morocco kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel unafuatia uamuazi sawa na huo uliochukuliwa miezi ya karibuni na Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain na Sudan. Nchi zingine za Kiarabu ambazo zina uhusiano rasmi na utawala bandia wa Israel ni Misri na Jordan.

Hatua ya madola hayo ya Kiarabu kuanzisha uhusiano na Israel inaendelea kulaaniwa kote duniani.

3943216/

 

captcha