IQNA

Maulid ya Mtume Muhammad (SAW)

Kiongozi Muadhamu atangaza msamaha kwa wafungwa kwa mnasaba wa Maulidi ya Mtume (SAW)

17:55 - October 13, 2022
Habari ID: 3475924
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameidhinisha pendekezo la kuachiwa huru au kupunguziwa vifungo wafungwa karibu 2,000 wa Kiirani, kwa mnasaba wa maadhimisho ya Maulidi ya Mtume (SAW) na kumbukumu ya mazazi ya Imam wa Ja'afar Swadiq (AS).

Ayatullah Sayyed Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameafiki pendekezo la Jaji Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Iran, Gholam Hossein Mohseni Ejei la kupunguziwa vifungo au kuachiwa huru wafungwa wapatao 1,862 wa Kiirani.

Kipengele cha 11 cha Sura ya 110 ya Katiba ya Iran kinampa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu haki ya kupunguza au kuwasamehe wafungwa kutokana na pendekezo la Jaji Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Iran.

Kesho tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiu Awwal mwaka 1444 Hijria kwa mujibu wa nukuu za maulama na wanahistoria wengi wa Kiislamu, itasadifiana na siku aliyozaliwa Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu, Muhammad bin Abdullah (SAW) na mjukuu wake mwema, Imam Ja'afar al Swadiq (AS).

Kuna kauli ya baadhi ya wanazuoni wa Kiislamu inayosema, Mtume Muhammad SAW alizaliwa tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal miaka 53 kabla ya Hijra. Kwa msingi huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitangaza kipindi cha kuanzia tarehe 12 hadi 17 Rabiul Awwal kila mwaka kuwa ni Wiki ya Umoja kati ya Waislamu kote duniani. 

Wiki ya Umoja ni fursa nzuri ya kuzikurubisha nyoyo za Waislamu na kuimarisha umoja na mshikamano wao katika kukabiliana na maadui wa ulimwengu wa Kiislamu.

4091594

 

captcha