IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Mapambano na mapigano makuu ni dhidi ya ubeberu wa kimataifa

21:13 - November 26, 2022
Habari ID: 3476153
TEHRAN (IQNA) -Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu mapema leo amehutubia hadhara kubwa ya wapiganaji wa kujitolea wa Basiji kwa mnasaba wa Siku ya Basiji ambako amesisitiza kuwa: Mapambano na mapigano makuu ni dhidii ya ubeberu wa kimataifa.

Katika kikao hicho cha Tehran kilichohudhuriwa na mamia ya wanachama wa Basij, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amekutaja kuundwa kwa taasisi ya Basiji kuwa ni miongoni mwa ubunifu muhimu na mkubwa zaidi wa Imam Ruhullah Khomeini (RA) na akasema: Mbinu muhimu zaidi inayotumiwa na wale wanaolitakia mabaya taifa la Iran ni kughushi na kueneza uongo ili kufikia malengo yao kwa kudhibiti bongo za watu.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Katika matukio ya hivi karibuni, Basiji waliodhulumiwa walijitosa katika medani ili taifa lisidhulumiwe mbele ya wafanya ghasia, watu walioghafilika au mamluki.

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: Eneo la Asia Magharibi ndilo kitovu kikuu cha mafuta, nishati na maliasili, na lina njia nne za mawasiliano kati ya Mashariki na Magharibi; kwa msingi huo utawala bandia na ghasibu wa Kizayuni ulianzishwa katika eneo hili la Magharibi mwa Asia ili nchi za Magharibi ziwe na kituo cha kupora rasilimali na kuanzisha vita na migawanyiko katika eneo hilo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, nukta muhimu na nyeti zaidi katika eneo la kistratijia la Asia Magharibi ni Iran na kubainisha kuwa: Kwa msingi huo, mwanzoni Waingereza na kisha Wamarekani walifanya uwekezaji maalumu kwa ajili ya kutengeneza mamluki nchini Iran, ili wawe na udhibiti kamili.

Amesema: Kwanza wanasema sitisheni urutubishaji wa asilimia 20 wa madini ya urani  kisha wanataka kusitishwa urutubishaji kwa kiwango cha asilimia 5 na baadaye wakataka kusitishwa sekta nzima ya nyuklia; baadaye walitaka kubadilishwa katiba ya nchi, kufungwa ndani ya mipaka ya Iran, kuipokonya kila kitu na kufungwa viwanda vya zana za ulinzi.

Ayatullah Ali Khamenei amesema: Mazungumzo na Marekani hayatatatua tatizo lolote, na Washington itaiachia Iran kama ilivyokuwa katika kipindi cha utawala wa kifalme wa Kipahlavi hapa nchini iwapo italegeza kamba katika masuala yote ya msingi na kuvuka mistari yake yote myekundu.

Amesisitiza kuwa: Makubaliano ya nyuklia ya JCPOA 2 yana maana kuwa Iran iachane kabisa na uwepo wake katika eneo hili la Magharibi mwa Asia, na JCPOA 3 ina maana kwamba Iran iahidi kutozalisha silaha zozote za kistratijia na muhimu kama vile makombora na ndege zisizo na rubani, ili iwe mikono mitupu mbele ya uvamizi ya adui.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria mpango uliofichuliwa na shakhsia wakubwa wa Marekani miaka 15 iliyopita na kusema: Mpango wao ulikuwa ni kuzipindua nchi sita za Iraq, Syria, Lebanon, Libya, Sudan na Somalia ili hatimaye kuharibu uwepo wa kistratijia wa Iran katika eneo hilo, na baada ya kudhoofika, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yenyewe pia hatimaye isambaratike.

Ayatullah Khamenei amesema, hata hivyo fikra na Mapinduzi ya Kiislamu yamekuwa na ufanisi katika nchi tatu za Iraq, Syria na Lebanon na kumefanyika kazi kubwa na muhimu, ambayo ilikuwa kushindwa kwa Marekani katika nchi hizo tatu.

Akiashiria kufeli kwa mipango ya Marekani ya kutaka kuangamiza harakati za Hizbullah na Amal huko Lebanon, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Mpango na njama hii iliyosukwa katika eneo hili ilizimwa na kuvunjwa na nguvu kubwa na madhubuti ya Jamhuri ya Kiislamu, na kielelezo na bendera ya nguvu hiyo kubwa ni shujaa aliyeitwa "Haj Qasim Soleimani"; kwa msingi huuo inaeleweka wazi ni kwa nini jina "Haj Qasim" linapendwa sana na watu wa Iran, na linawakosesha raha kwa kiwango hicho maadui wa taifa hili.

 

4102351

Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha