IQNA

Njama dhidi ya Iran

Kiongozi Muadhamu: Tarehe 13 Aban inadhihirisha uovu, ukhabithi na kushindwa Marekani

18:05 - November 02, 2022
Habari ID: 3476025
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, tarehe 13 Aban (Novemba 4) ni mfano wa wazi wa uovu, ukhabithi na dhihirisho la kupata pigo na kushindwa Marekani.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema hayo leo mbele ya hadhara ya wanafunzi kwa mnasaba wa kukaribia kumbukumbu ya “Siku ya Kupambana na Ustikbari wa Kimataifa na Siku ya Mwanafunzi hapa Iran na kusisitiza kwamba, 13 Aban ni siku ya kihistoria na wakati huo ho ni siku ya kujipatia na kujifunza tajiriba.

Katika hotuba yake, Ayatullah Ali Khamenei ameitaja tarehe 13 Aban (4 Novemba) kuwa ni siku ya kihistoria na yenye ibra na  mafunzo. Ameashiria tukio la kupelekwa uhamishoni Imam Ruhullah Khomeini, mauaji ya idadi kubwa ya wanafunzi mbele ya Chuo Kikuu cha Tehran na shambulio la wanafunzi kwenye Ubalozi wa Marekani tarehe 4 Novemba 1979, na kusema: "Wamarekani na wenye mielekeo ya Kimarekani wana hasira na ghadhabu kuhusu siku hii muhimu na mikusanyiko yake inayojenga umoja; kwa sababu siku hii ni kielelezo cha maovu ya Marekani na uthibitisho wa udhaifu na uwezekano wa kushindwa kwake."

Ayatullah Khamenei amewahutubu wanafunzi hao na kuwataka wajifunze tajiriba hii na mustakabali wao.

Kiongozi Muadhamu amesema kuwa, watu wanaodhani kwamba, Marekani ni nguvu isiyotikisika, tukija na kuangalia na kutupia jicho matukio ya siku hii tunaona kwamba, hapana, dola hilo la kibeberu linaweza kudhurika na kupata pigo.

Ayatullah Khamenei ameashiria mahesabu kombo ya Marekani katika matukio mbalimbali kama huko Afghanistan na Iraq na kubainisha jinsi siasa za Marekani zilivyojengwa juu ya misingi ya unafiki na kutokuwa na haya wala soni.

Kiongozi Muadhamu ameashiria shambulio la kigaidi la hivi karibuni dhidi ya Haram takatifu ya Ahmad bin Musa (as) huko katika mji wa Shiraz na kueleza kuwa, mauaji dhidi ya wasio na watoto wasio na hatia ni jinai kubwa, hivyo waliohusika na jinai hiyo wanapaswa kutambuliwa na kuadhibiwa pamoja na mtu yeyote ambaye itathibiti alitoa ushirikiano katika jinai hiyo kwa namna moja au nyingine.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia kuhusika kwa Marekani katika machafuko ya wiki chache zilizopita nchini Iran na kusema: "Taarifa ya pamoja la Wizara ya Usalama wa Ndani na Shirika la Upelelezi la Jeshi la Walinzi waMapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kuhusu machafuko hayo imekusanya habari na uvumbuzi muhimu na inaonyesha kuwa adui alikuwa amepanga njama kwa ajili ya Tehran na miji mikubwa na midogo hapa nchini."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia ameyataja maneno ya wanasiasa wa Marekani siku hizi kuhusu kulipenda taifa la Iran kuwa ni kilele cha ukosefu wa haya na unafiki: Akibainisha nukta hiyo Kiongozi Muadhamu alisema: "Wanasiasa wa Marekani kwa kufanya Mambo kwa kujionyesha na bila haya wanasema katika vyombo vya habari kwamba wanawaunga mkono wananchi wa Iran. Madai hayo ni ya aibu kabisa. Swali langu kwa Wamarekani ni hili; je katika miongo minne iliyopita ni mambo gani ambayo mungeweza kuyafanya dhidi ya taifa la Iran na hamukuyafanya? Yale ambayo hawakuyafanya dhidi ya taifa la Iran ni yale ambayo hawakuwa na uwezo wa kuyafanya. Kama wangeweza na hawakuwaogopa vijana wa Iran wangeyafanya. Wangeanzisha vita vya moja kwa moja dhidi ya Iran kama walivyoanzisha dhidi ya Iraq lakini waliogopa."

 Ayatullah Ali Khamenei pia ameashiria uongo mkubwa wa Wamarekani kwamba eti wanalionea huruma taifa la Iran na kusisitiza kuwa: "Katika vita mseto vya wiki chache zilizopita, Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel, baadhi ya madola ya Ulaya na makundi washirika yametumia rasilimali zao zote kwa ajili ya kutoa pigo dhidi ya taifa la Irani, lakini taifa limetoa dhoruba kali kwa wasiolitakia mema na kutibua mipango yao."

Tarehe 13 Aban 1358 Hijria Shamsia iliyosadifiana na tarehe 4 Novemba 1979, wanafunzi wa Chuo Kikuu wa Iran walilivamia pango la kijasusi la Marekani mjini Tehran lililokuwa na ubalozi wa dola hilo la kibeberu baada ya kuongezeka njama za Marekani za kutaka kufanya mapinduzi mengine nchini Iran.

4096407

captcha