IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Lengo la waibua ghasia Iran lilikuwa ni kuharibu nguvu za nchi na si kuondoa udhaifu

23:17 - January 09, 2023
Habari ID: 3476379
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyataja matukio ya mabadiliko ya historia kuwa yana uzoefu mkubwa wa kujifunza au yanaashiria sunna ya Mwenyezi Mungu.

Ayatullah Sayyed Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo asubuhi amekutana hapa mjini Tehran na wakazi wa mji wa Qum sambamba na maadhimisho ya kukumbuka mapambano ya kihistoria ya watu watu wa mji huo mnamo tarehe 19 mwezi Dei mwaka 1356 Hijria Shamsiya iliyosadifiana na Januari 9 mwaka 1978 ambapo amesema: ni jambo la dharura kubakisha hai na kujifunza kutokana na tukio adhimu la tarehe 19 Dei mwaka 1356 Hijiria Shamsiya huko Qum na kubainisha kuwa mapambano adhimu ambayo yalianza kote nchini kwa bendera za wananchi waumini na wanamapinduzi wa mji wa Qum yalikuwa na lengo la kuung'oa madarakani utawala wa kidikteta, kuitoa Iran katika tumbo la Wamagharibi na kuhuisha utambulisho wa kihistoria na Kiislamu wa nchi hii. Hii ni kwa sababu Iran katika zama za utawala wa Pahlavi ilikandamizwa chini ya mikono na miguu ya tamaduni potofu na utawala wa kisiasa na kijeshi wa Wamarekani. 

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la Kujihami Kutakatifu kuwa mfano unaong'ara wa wananchi kuhisi majukumu waliyonayo, kufika kwa wakati na kujiweka hatarini na kueleza kuwa: Saddam dikteta aliyepinduliwa wa Iraq aliishambulia Iran kwa kustafidi na suhula chungu nzima na kwa kuungwa mkono kwa pande zote na Marekani, Umoja wa Kisovieti, NATO na nchi nyingine vibaraka lengo likiwa ni kuigawa nchi hii; hata hivyo Iran iliibuka na ushindi katika vita hivyo vya makundi; na wao hawakuthubutu kufanya lolote na hata hakuna hata sehemu moja ya nchi iliyotenganishwa na ardhi mama ya Iran. Ayatullah Khamenei ameutaja pia Ushindi wa Mapinduzi na kukombolewa Iran katika udhibiti mkubwa wa Marekani kuwa sababu kuu ya nchi hiyo kuwa na uadui na uhasama na mfumo wa Kiislamu. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha ameashiria hatua ya kituo kimoja kinachotambulika cha nchini Marekani ya kuchapishwa nyaraka za siri kuhusu amri iliyotolewa na Rais wa wakati huo wa Marekani Jimmy Carter kwa ajili ya kuing'oa madarakani Jamhuri ya Kiislamu tena wakati huo ikiwa imepita miezi 10 tu baada ya Ushindi wa Mapinduzi na kueleza kuwa: kwa mujibu wa nyaraka hizo, Carter aliliamuru Shirika la Ujasusi CIA kuipindua Jamhuri ya Kiislamu; ambapo stratejia ya kwanza aliyoitaja ili kuweza kuipindua Jamhuri ya Kiislamu ni kustafidi na wenzo wa propaganda. 

Katika sehemu nyingine ya mazungumzo kati yake  na wakazi wa mji wa Qum, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia pia lengo la waliopanga machafuko na ghasia za karibuni hapa nchini na kusema: mkono wa adui ajinabi umeonekana wazi kikamilifu katika matukio hayo; na si sahihi kwamba baadhi ya watu wanapinga uingiliaji wa adui ajinabi na kusema kuwa matukio hayo ni makosa yenu."  

4113280

captcha