IQNA

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Mustakbali wa maendeleo ya Iran ni angavu zaidi kuliko utabiri wa hivi sasa

18:33 - January 30, 2023
Habari ID: 3476491
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema katika kikao chake na mamia ya wazalishaji, wajasiriamali na wanaharakati katika nyuga zinazoegemea elimu kuwa, mustakbali wa taifa na matarajio ya maendeleo ya Iran ni angavu zaidi kuliko utabiri wa hivi sasa.

Katika kikao hicho kilichofanyika leo Jumatatu mjini Tehran, Ayatullah Sayyed Ali Khamenei ameeleza kufurahishwa kwake na ari, mtazamo wa matumaini na shughuli zinazoonekana za wanaharakati wa uzalishaji na ujasiriamali wa Iran na kusema kuwa, talanta na uwezo wa ustawi wa taifa kwa kutilia maanani rasilimali za nchi, nafasi ya kijiografia, kimataifa na kisiasa hasa rasilimali watu, ni wa juu na wa kipekee katika baadhi ya nyuga, na kwa sababu hii, mustakbali wa taifa na dira ya maendeleo ya Iran ni angavu zaidi kuliko utabiri wa sasa.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema mustakbali mwema wa Iran unahitajia ukuaji wa haraka na endelevu wa uchumi. Ameashiria kipaumbele cha maendeleo ya kiuchumi sambamba na kuchunga uadilifu katika mpango wa 7 wa maendeleo ya taifa na kueleza sababu na masharti ya ustawi wa uchumi. Vilevile amesisitiza kuwa, utatuzi wa matatizo ya kimaisha ya wananchi unazidisha udharura wa kuwepo ustawi wa kiuchumi.

Ayatullah Khamenei amesema, jina la mwaka huu wa Hijria Shamhsia ambalo ni "Mwaka wa Uzalishaji Unaotegemea Elimu na Kutengeneza Ajira" kwa kiasi fulani lilitokana na mkutano wa mwaka jana na wanaharakati wa masuala ya kiuchumi na kuongeza kuwa: Maonyesho yaliyotembelewa siku mbili zilizopita yalionesha kwamba kumechukuliwa hatua nzuri katika uwanja wa kauli mbiu ya mwaka huu. Ameongeza kuwa matamshi ya wanaharakati wa uchumi katika mkutano wa leo pia kuhusiana na maendeleo ya kiuchumi ya nchi yanatoa matumaini na bishara nzuri, na kwamba viashiria rasmi vya nusu ya kwanza ya 1401 vinaashiria kuwepo harakati na ustawi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema mafanikio ya sasa katika sekta nyingi ni matokeo ya harakati ya kisayansi ya takriban miaka kumi na tano iliyopita na kuongeza kwamba, wanasayansi chipukizi wanapaswa kuvuka mstari wa mbele wa sayansi na elimu duniani na waweke msingi mzuri wa kutimizwa azma hiyo kiasi kwamba, miaka hamsini baadaye ikiwa mtu atataka kujua sayansi mpya, alazimike kujifunze lugha ya Kiajemi (Kifarsi).

4118260

captcha