Uyahudi ni miongoni mwa dini ambazo zinatajwa kuwa za Ibrahimu ambayo nabii wake ni Musa (AS) na kitabu chake kitakatifu ni Torati.
Katika Qur'ani Tukufu, Mayahudi hawakutambulishwa kama kabila bali kama kundi la kidini, wakati Bani Isra’il wanatajwa kuwa ni kaumu
Mtazamo wa Qur'ani Tukufu juu ya Mayahudi ni hasi kiasi, lakini Bani Isra’il ni watu ambao Qur'ani Tukufu inawatazama kutoka pembe tofauti.
Bani Isra’il walikuwa ni watu wa dhuria wa wale waliopanda katika safina ya Nabii Nuhu. Na tukampa Musa Kitabu, na tukakifanya uwongofu kwa Wana wa Israili. (Tukawambia): Msiwe na mtegemewa ila Mimi! Enyi kizazi tuliyo wachukua pamoja na Nuhu! Hakika yeye alikuwa mja mwenye shukrani.” Aya 2-3 ya Suratul Israa.
Walikuwa ni kizazi cha Nabii Yaqub (Yakub) waliochaguliwa na Mwenyezi Mungu miongoni mwa wengine wote. " Enyi Wana wa Israili! Kumbukeni zile neema zangu nilizo kuneemesheni, na nikakuteuweni kuliko wote wengineo." Aya ya 47 ya Surah Al-Baqarah.
Mwenyezi Mungu aliwateremshia kitabu Chake, pamoja na wengi wa Mitume Wake – kutoka kwa Musa (AS) hadi kwa Isa (AS) kwao, na akawateremshia ishara zake nyingi.
"Waulize Wana wa Israili: Tumewapa ishara ngapi zilizo wazi? Na anaye zibadili neema za Mwenyezi Mungu baada ya kumfikia basi hakika Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu." Aya ya 211 ya Surah Al-Baqarah.
Walitarajiwa kubaki kujitolea kwa ahadi waliyoweka na Mungu. "Enyi Wana wa Israili! Kumbukeni neema yangu niliyo kuneemesheni, na timizeni ahadi yangu, na Mimi nitatimiza ahadi yenu, na niogopeni Mimi tu." Aya ya 40 ya Surah Al-Baqarah
Lakini walifanya nini? Walivunja ahadi yao, wakaanza kuabudu masanamu na kumwacha Musa (AS) peke yake.
Na pale Musa alipo waambia watu wake: Enyi watu wangu! Kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu zilizo juu yenu, alipo wateuwa Manabii kati yenu, na akakufanyeni watawala, na akakupeni ambayo hakuwapa wowote katika walimwengu.
Enyi watu wangu! Ingieni katika nchi takatifu ambayo Mwenyezi Mungu amekuandikieni. Wala msirudi nyuma, msije mkawa wenye kukhasirika. Wakasema: Ewe Musa! Huko wako watu majabari. Nasi hatutaingia huko mpaka wao watoke humo.
Wakitoka humo hapo tutaingia. Watu wawili miongoni mwa wachamngu ambao Mwenyezi Mungu amewaneemesha, walisema: Waingilieni kwa mlangoni. Mtakapo waingilia basi kwa yakini nyinyi mtashinda. Na mtegemeeni Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi ni Waumini.
Wakasema: Ewe Musa! Sisi hatutaingia humo kamwe maadamu wao wamo humo. Basi nenda wewe na Mola wako Mlezi mkapigane. Sisi tutakaa hapa hapa.
Akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika mimi similiki ila nafsi yangu na ndugu yangu. Basi tutenge na hawa watu wapotovu.
(Mwenyezi Mungu) akasema: Basi nchi hiyo wameharimishiwa muda wa miaka arubaini, watakuwa wakitanga-tanga katika ardhi. Basi wewe usiwasikitikie watu wapotovu. Aya ya 20-26 ya Surah Al-Ma’idah
Waliacha kitabu cha Mwenyezi Mungu na wakawakanusha Mitume na wakawaua baadhi yao.
Tulifanya agano na Wana wa Israili, na tukawatumia Mitume. Kila alipo wajia Mtume kwa wasio yapenda nafsi zao wengine waliwakanusha na wengine wakawauwa. Aya ya 70 ya Surah Al-Ma’idah.
Na mwishowe wakawa ni Makafir kwa dini yenyewe hivyo “walilaaniwa walio kufuru katika Wana wa Israili kwa ulimi wa (Mitume) Daudi na Isa.”
Walilaaniwa walio kufuru miongoni mwa Wana wa Israili kwa ulimi wa Daud na wa Isa mwana wa Maryamu. Hayo ni kwa sababu waliasi na wakawa wanapindukia mipaka. Aya ya 78 ya Surah Al-Ma’idah.
Hata hivyo, Mungu hangewaangamiza na aliweka njia wazi kwa ajili yao ya kurejea kwenye rehema yake.
"Huenda Mola wenu Mlezi akakurehemuni. Na mkirudia na Sisi tutarudia. Na tumeifanya Jahannamu kuwa ni gereza kwa ajili ya makafiri." (Aya ya 8 ya Surah Al-Isra)