IQNA

Hali nchini Syria

Wabunge wa nchi za Kiarabu watembelea Damascus kuonyesha mshikamano na Wasyria

6:39 - February 27, 2023
Habari ID: 3476631
TEHRAN (IQNA)- Ujumbe wa maspika na wabunge wa mabunge ya nchi za Kiarabu uliwasili Damascus, mji mkuu wa Syria siku ya Jumapili kuonyesha mshikamano na nchi hiyo kufuatia matetemeko makubwa ya ardhi yaliyosababisha vifo vya maelfu ya watu nchini Syria na Uturuki.

Ziara hiyo ni ya aina yake ni ya kwanza tangu mwaka 2011 wakati Jumuiya ya Nchi za Kiarabu yenye makao yake mjini Cairo ilipositisha kwa muda uanachama wa Syria.

Taarifa zinasema Spika wa Bunge la Misri Hanafi Al-Gebali aliwasili Damascus kama sehemu ya ujumbe wa bunge la Kiarabu kuonyesha mshikamano na Syria kufuatia tetemeko la ardhi.

Masipka wa mabunge ya Iraq, Umoja wa Falme za Kiarabu, Libya, Jordan na Palestina halikkadhalika walikuwa katika ujumbe huo uliokaribishwa na Rais wa Syria Bashar al-Assad.

Rais AssadAssad alisema ziara hiyo inaonyesha kuna taasisi za Kiarabu ambazo bado zina uwezo wa kuchukua hatua kwa maslahi ya Waarabu. Aidha amezishukuru nchi hizo kwa mwitikio wao wa haraka katika kuwasaidia wananchi wa Syria kufuatia matetemeko la ardhi.

Shirika la habari la serikali ya Iraq INA limesema Spika wa Bunge Mohammed al-Halbousi amesema "Wajumbe hao wanawakilisha Umoja wa Mabunge ya Kiarabu ili kubainisha uungaji mkono kwa Syria na kusimama na watu wake katika masaibu yaliyosababishwa na matetemeko ya ardhi."

Takriban watu  zaidi ya 50,000 hadi sasa wamethibitishwa kupoteza maisha katika matetemeko mawili makubwa ya ardhi yaliyokumba Uturuki na Syria mnamo Februari 6. Idadi ya watu waliopoteza maisha Uturuki hadi sasa ni 44,218 huku waliopoteza maisha Syria wakiwa ni 5,914.

Matetemeko ya ardhi yenye ukubwa wa 7.7 na 7.6, yaliyojikita katika mkoa wa Kahramanmaras, yaliathiri zaidi ya watu milioni 13 katika majimbo 11, yakiwemo Adana, Adiyaman, Diyarbakir, Gaziantep, Hatay, Kilis, Malatya, Osmaniye, Elazig na Sanliurfa.

3482625

captcha