IQNA

Uchambuzi

Kufunguliwa tena ubalozi wa Iran nchini Saudi Arabia ni ishara ya kufeli sera za Marekani

19:33 - June 08, 2023
Habari ID: 3477121
Sambamba na kufufuliwa uhusiano wa kisiasa na kidiplomasia kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Ufalme wa Saudi Arabia, ubalozi wa Iran mjini Riyadh ulifunguliwa tena Jumanne, Juni 6 baada ya kufungwa kwa miaka saba.

Alireza Bigdeli, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayshughulikia Masuala ya Kibalozi  alisema katika hotuba yake katika sherehe za ufunguzi huo kwamba: "Leo ni siku muhimu katika historia ya uhusiano kati ya nchi hizi mbili. Tunayo furaha kubwa kuwepo katika nchi hii ndugu na rafiki ya Saudi Arabia. "Bigdeli alisema kuwa kwa kupandishwa bendera za Saudi Arabia na Iran katika nchi hizo mbili, ushirikiano wa pande mbili utafikia kilele chake. Aidha ameongeza kuwa: "Tunashuhudia ukurasa mpya katika uhusiano wa nchi hizi mbili. Mahusiano baina ya nchi mbili na kikanda yanaelekea kwenye ushirikiano na mshikamano zaidi."

Kufunguliwa tena ubalozi wa Iran nchini Saudi Arabia ni hatua mpya kuelekea kurejesha uhusiano wa kawaida wa kisiasa na kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili muhimu za Asia Magharibi katika Ghuba ya Uajemi na kuwa msingi wa kustawisha uhusiano kati ya nchi hizo katika nyanja zote.

Kufunguliwa tena kwa ubalozi wa Iran huko Riyadh kumefanyika kufuatia makubaliano ya Machi 10, 2023 kati ya Iran na Saudi Arabia huko Beijing chini ya upatanishi wa China. Katika mapatano hayo nchi hizi mbili zilikubali kuanzisha tena uhusiano wa kidiplomasia baada ya kukatwa kwa miaka saba.

Tuhuma zisizo na msingi za Marekani

Licha ya Marekani kuonekana kuwa na msimamo mzuri wa awali katika uga wa kurejeshwa uhusiano wa kawaida kati ya Iran na Saudi Arabia, Washington imeendelea kuishutumu Tehran ikiwa ni pamoja na kuleta hali ya wasiwasi katika eneo la Magharibi mwa Asia.

Makubaliano ya hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa muungano wa baharini kati ya Iran na nchi za mwambao wa kusini mwa Ghuba ya Uajemi, yamepingwa na Marekani. Kuhusiana na hilo, "Tim Hawkins", msemaji wa Msafara wa Tano wa Meli za Kivita za Jeshi la Wanamaji la Marekani, amepinga kuundwa kwa muungano wa pamoja wa Jeshi la Wanamaji la Iran na nchi za eneo zikiwemo Saudi Arabia, Imarati, Qatar, Bahrain na Iraq na kudai kwamba eti “muungano huo hauendani na vitendo vya Iran.”

Msimamo huo unaonyesha kwamba Marekani, licha ya propaganda za chuki dhidi ya Iran katika miongo michache iliyopita, sasa inajikuta katika hali ya hatari ya kufeli siasa zake za nje dhidi ya Iran. Kwa hakika mchakato wa kurejesha uhusiano wa kawaida kati ya Iran na nchi za Kiarabu ni kinyume na matakwa ya Washington na Tel Aviv ambazo zilikuwa na matumaini makubwa ya kuendelea na mchakato wa kurejesha uhusiano wa kawaida wa nchi za Kiarabu na utawala haramu wa Israel ili kuunda muungano dhidi ya Iran. Sasa kinyume na matarajio ya Marekani, kunashudiwa muungano mpya wa Iran na nchi za Kiarabu.

Inaonekana kuwa wasiwasi wa kupanuka mchakato wa kurejeshwa uhusiano wa kawaida kati ya Iran na Saudi Arabia na kujaribu kufufua mchakato wa kurejesha uhusiano wa Riyadh na Tel Aviv ni moja ya sababu kuu za ziara ya hivi sasa ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Anthony Blinken huko Saudia ambapo amekutana na Mrithi wa Ufalme wa nchi hiyo, Mohammed bin Salman.

Si muda mrefu uliopita, tovuti ya Marekani ya Axios iliripoti kuwa "Mohammed bin Salman" amekataa ombi la Ikulu ya White House la kutaka kurudisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.  Aidha, safari ya Blinken imefanyika katika hali ambayo serikali ya Biden inakusudia kuleta utulivu katika uhusiano wa Washington na Riyadh.

Uhusiano kati ya Marekani na Saudia umekumbwa na mivutano mbalimbali kutokana na hitilafu katika masuala kadhaa, kuanzia kurejesshwa  uhusiano  wa kawaida na Iran hadi bei ya mafuta ya petroli hasa sisitizo la Saudia la kupunguza uzalishaji wa mafuta ndani ya fremu ya makubaliano ya OPEC+.

4145904

captcha