IQNA

Ulimwengu wa Kiislamu

Iran na Saudi Arabia zaafikiana kurejesha uhusiano wa kidiplomasia

21:14 - March 10, 2023
Habari ID: 3476685
TEHRAN (IQNA)-Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Saudi Arabia zimefikia makubaliano ya kurejesha uhusiano wao wa kidiplomasia na kufungua tena balozi, miaka saba baada ya kuvunjika uhusiano huo kutokana na masuala kadhaa.

Makubaliano hayo yaliafikiwa Ijumaa katika mji mkuu wa China, Beijing, baada ya siku kadhaa za mazungumzo magumu kati ya Katibu wa Baraza Kuu la Usalama la Taifa la Iran (SNSC) Ali Shamkhani na mwenzake wa Saudia.

Kurejeshwa kwa uhusiano huo kulitangazwa rasmi katika taarifa ya pamoja ya Iran, Saudi Arabia na China siku ya Ijumaa.

Mapatano hayo yalisainiwa na Shamkhani, Musaid Al Aiban, Waziri wa Nchi na mjumbe wa Baraza la Mawaziri wa Saudi Arabia ambaye pia ni  Mshauri wa Usalama wa Taifa, na Wang Yi Mkurugenzi wa Ofisi ya Kamisheni Kuu ya Mambo ya Nje ya Chama cha Kikomunisti cha China.

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema: "Kutatua hitilafu na kuangalia mustakbali wa uhusiano wa Tehran na Riyadh bila shaka kutapelekea kustawishwa kwa uthabiti na usalama wa eneo na kuongezwa ushirikiano kati ya nchi za Ghuba ya Uajemi na ulimwengu wa Kiislamu katika kusimamia changamoto zilizopo."

Kufuatia mazungumzo kati ya Rais wa Iran Ebrahim Raisi na mwenzake wa China Xi Jinping mjini Beijing mwezi Februari, Shamkhani alifanya mazungumzo ya kina na mwenzake wa Saudia mjini Beijing tangu Jumatatu ili kutafuta suluhu la mwisho la masuala kati ya Tehran na Riyadh.

Akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo, Shamkhani alisema mazungumzo kati ya nchi hizo mbili yalikuwa "ya wazi, ya uwazi na ya kina."

Amesema, "kuondoa hitilafu na kuangalia mustakabali wa uhusiano wa Tehran na Riyadh bila shaka kutapelekea kustawi kwa uthabiti na usalama wa eneo na kuzidisha ushirikiano kati ya nchi za Ghuba ya Uajemi na Ulimwengu wa Kiislamu ili kudhibiti changamoto zilizopo."

Saudi Arabia ilikata uhusiano wa kidiplomasia na Iran mnamo Januari 2016 baada ya waandamanaji wa Iran, waliokasirishwa na hatua ya Saudia kumyong kiongozi mashuhuri wa Kishia Sheikh Nimr kuvamia ubalozi wake mjini Tehran.

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama la Kitaifa la Iran alitathmini duru 5 za mazungumzo ya awali kati ya Iran na Saudi Arabia ambayo yaliandaliwa na Iraq na Oman kuwa yenye ufanisi katika kufikia makubaliano ya mwisho na kuongeza kuwa nchi hizo mbili za Kiarabu zilikuwa na nafasi muhimu katika kufikiwa mapatano.

Kwa mujibu wa makubaliano ya nchi hizo mbili, mawaziri wa mambo ya nje wa Iran na Saudi Arabia watakutana ndani ya miezi miwili ili kuainisha misingi ya utekelezaji wa mabadilishano ya mabalozi na kufunguliwa kwa balozi, kati ya mambo mengine.

3482753

captcha