IQNA

Kadhia ya Palestina

Waziri Mkuu wa Libya asisitiza kuunga mkono kadhia ya ukombozi wa Palestina

19:54 - September 01, 2023
Habari ID: 3477534
TEHRAN (IQNA)- Baada ya maandamano makubwa ya wananchi wa Libya kulaani kikao cha Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo na Waziri wa Mambo ya Nje wa utawala haramu wa Israel, Waziri Mkuu wa Libya amesema: Tripoli inaunga mkono suala la ukombozi wa Palestina.

Abdul Hamid al-Dbeibeh, Waziri Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya yenye makao yake Tripoli, Alhamisi jioni kwa mara nyingine alisisitiza uungaji mkono wa nchi hiyo kwa suala la Palestina na mapambano ya kupigania ukombozi Wapalestina dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Waziri Mkuu wa Libya pia amesema: Tunapinga kuanzisha uhusiano wowote na Israel.

Jumapili iliyopita vyombo vya habari vya Israel viliripoti kuhusu kikao cha siri kati ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Tel Aviv, Eli Cohen na Waziri wa Mambo ya Nje wa Libya Najla Al-Mangoush huko Roma, Italia, kilichofanyika katika hatua ya kwanza kwa lengo la kujadili uhusiano kati ya utawala wa Kizayuni na Libya.

Baada ya kufichuliwa kwa mkutano huo na vyombo vya habari vya Kizayuni, maandamano mengi yalifanyika katika miji ya Libya kuupinga, ambapo waandamanaji walichoma moto bendera ya Israel na kufunga barabara za miji kadhaa ya Libya.

Jumatatu iliyopita, al-Dbeibeh alimuondoa rasmi  Al-Mangoush kwenye nafasi yake.

Al-Mangoush alikiri kuwa alifanya mazungumzo na Eli Cohen kwa uratibu wa waziri wa mambo ya nje wa Italia, Antonio Tajani, lakini amedai kuwa mazungumzo hayo hayakuwa rasmi na kwamba hakuna makubaliano yoyote yaliyofikiwa.

Inadokezwa kuwa Al Mangoush sasa amekimbilia Uturuki baada ya Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya kumsimamisha kazi.

Baadhi ya viongozi na wanasiasa mashuhuri wa Libya wametoa mwito wa kuondolewa mamlakani serikali nzima ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo baada ya kashfa hiyo ya mkutano wa Al Mangoush na Waziri mzayuni.

Khalid al-Mishri, Mwenyekiti wa zamani wa Baraza Kuu la Uongozi la Libya amelaani mkutano baina ya wawili hao ambao anasisitiza kuwa, yumkini si wa kwanza kufanyika.

3484999

Habari zinazohusiana
captcha