IQNA

Diplomasia ya Kiislamu

Balozi wa Iran akutana na Waziri wa Masuala ya Kiislamu wa Saudia mjini Riyadh

18:13 - December 19, 2023
Habari ID: 3478060
IQNA - Balozi wa Iran mjini Riyadh alikutana na Waziri wa Masuala ya Kiislamu wa Saudia Jumatatu na kujadili uhusiano kati ya nchi hizo mbili na changamoto zinazoukabili ulimwengu wa Kiislamu.

Alireza Enayati, Balozi wa  Iran  mjini Riyadhe amesema kuwa, Iran na Saudi Arabia ni nchi mbili muhimu katika ulimwengu wa Kiislamu na kwamba uhusiano wao wa kindugu umesaidia kukuza nafasi ya nchi za Kiislamu katika maendeleo ya kimataifa kwa mujibu wa taarifa ya ubalozi wa Iran.

Vile vile amesema nchi za Kiislamu zinapaswa kushikamana katika kukabiliana na changamoto za nje na kufanya kazi pamoja kwa ajili ya maslahi ya pamoja ya Umma wa Kiislamu.

Sheikh Abdullatif bin Abdulaziz Al-Sheikh, Waziri wa Masuala ya Kiislamu wa Saudi Arabia alimkaribisha balozi wa Iran na kuashiria juhudi zinazofanywa na uongozi wa Saudia katika kuutumikia Uislamu na Waislamu.

Alisema wizara yake inataka, kupitia programu zake mbalimbali, kudhihirisha kuwa Uislamu ni dini ya wastani na inatoa wito wa kuishi pamoja na kuhurumiana kati ya watu wote.

Enayati alipongeza juhudi za Saudia za kueneza Uislamu wa wastani na kuhudumia dini, mahujaji, maeneo matakatifu, na misikiti miwili mitakatifu ya Makka na Madina.

Aidha ameipongeza wizara hiyo kwa kuhimiza watu kujihusisha na Qur'ani Tukufu ikiwa ni pamoja na mashindano ya kusoma na kuhifadhi  kitabu hicho Kitukufu na pia  kutunza misikiti.

Mkutano huo ulikuwa sehemu ya mfululizo wa mawasiliano ya kidiplomasia kati ya Iran na Saudi Arabia, ambayo yalianza kwa kuhuishwa  tena uhusiano wao wa kidiplomasia Machi 2023 kupitia makubaliano yaliyosimamiwa na China.

Habari zinazohusiana
captcha