IQNA

Watetezi wa Qur'ani Tukufu

Mapendekezo ya Iran kwa ajili ya kukabiliana na vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu

17:32 - August 01, 2023
Habari ID: 3477369
TEHRAN (IQNA)- Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Hossein Amir Abdollahian amewasilisha mapendekezo ya Iran kwa ajili ya kukabiliana na vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika nchi za Ulaya.

Mapendekezo hayo yamewasilishwa katika kikao cha dharura cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, OIC.

Akihutubia Mkutano wa 18 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu ulifanyika kwa njia ya video (mtandaoni), Hossein Amir Abdollahian alisema: "Kikao cha leo kinapaswa kuwa mwendelezo wa juhudi za awali za nchi wanachama wa OIC katika kukabiliana na matusi na vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu na maadili ya dini ya Kiislamu.

Ameongeza kuwa: "Mkutano wa leo unaonyesha azma thabiti ya nchi za Waislamu, kama wawakilishi wa Umma mmoja wa Kiislamu, kukabiliana ipasavyo na propaganda chafu dhidi ya Uislamu, chuki, ubaguzi na unyanyasaji sio tu dhidi ya Waislamu, bali pia dhidi ya imani, itikadi, maadili na matakatifu na dini nyenginezo za Mwenyezi Mungu.

Amir Abdollahian amesema: "Inasikitisha kuona kwamba, mwenendo unaoongezeka wa kutovumiliana na ukatili dhidi ya Uislamu na Waislamu katika baadhi ya nchi za Ulaya umekuwa changamoto kubwa kutokana na uungaji mkono wa baadhi ya mirengo inayotawala' jambo ambalo si la kibinadamu."

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran amesema: Kitendo cha kejeli, matusi na kuibua chuki cha kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu, kubeza thamani za kibinadamu na itikadi takatifu zaidi za Waislamu zaidi ya bilioni 2 duniani kote, ni dhihirisho jingine la mwenendo unaotia wasiwasi mkubwa.

Abdollahian amesema: Tunaamini kuwa hatua za kuzuia kukaririwa dharau na kuvunjiwa heshima matukufu ya dini, ikiwemo dini ya Uislamu, ina manufaa kwa watu wote, na matukio machungu ya hivi majuzi huko Uswidi na Denmark yanazipa nchi za Kiislamu jukumu la pamoja la kuzishinikiza serikali za Ulaya kuchukua hatua za kukomesha vitendo hivyo vya uchochezi haraka iwezekanavyo, na kuwawajibisha wahusika wa uhalifu huu kwa mujibu wa sheria na kuwaadhibu vikali.

Miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuitaka Majlisi ya Sheria ya Kiislamu ya OIC kushughulikia kwa dharura suala hili muhimu katika ajenda ya kuharamisha vitendo hivyo viovu katika ngazi ya kitaifa, kieneo na kimataifa, na pia kuanzisha mazungumzo baina ya dini tofauti na viongozi wa kidini nchini Uswidi na Denmark au hata katika ngazi ya Umoja wa Ulaya ili kurekebisha hali ya sasa.

4159531

captcha