IQNA

Mkutano wa Fiqhi wamalizika Qatar, ukitoa Fatwa kuhusu Akili Mnemba, Michezo ya Kidijitali, Afya ya Akili na Haki za Watoto

21:26 - May 09, 2025
Habari ID: 3480661
IQNA – Kikao cha 26 cha Chuo cha Kimataifa cha Fiqhi ya Kiislamu (IIFA) kimehitimishwa jijini Doha baada ya siku tano za mijadala, kikitoa mapendekezo muhimu kuhusu akili mnemba (AI), michezo ya kidijitali, afya ya akili, na ustawi wa watoto.

Mkutano huu ulijadili masuala kadhaa ya kisasa yenye umuhimu wa dharura, yakiwemo ustawi wa watoto, kanuni ya kifiqhi ya istishab (kuendeleza hali ya awali hadi ithibitike vinginevyo) na matumizi yake ya sasa, pamoja na hukumu na maadili yanayohusiana na akili mnemba, michezo ya kidijitali, na malipo ya riba kwa mkopo wa mtu wa tatu.

IIFA ikiwa chini ya mwavuli wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), ilisisitiza kwamba wajibu wa kuwalinda na kuwalea watoto ni wa familia, jamii na dola kwa pamoja, kwa mujibu wa sheria na maadili. Chuo hicho kimehimiza kulinda utambulisho wa Kiislamu na kitaifa wa watoto.

Mapendekezo ya mkutano yalitilia mkazo ulinzi wa watoto dhidi ya aina zote za madhara, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kimwili na kihisia, vitisho, dhuluma, matusi, unyanyasaji wa kijinsia, unyanyasaji wa kimtandao, na vurugu za aina yoyote. Pia, wazazi walihimizwa kuwajibika kuwalinda watoto wakati wa vita, mizozo ya silaha, na wakimbizi, huku ikisisitizwa umuhimu wa kulinda utambulisho wa kijinsia wa mtoto ili kuhakikisha maendeleo yake ya kiasili.

Aidha, Chuo cha Kimataifa cha Fiqhi ya Kiislamu kilisisitiza umuhimu wa kuwalea watoto kwa misingi ya maadili mema na kuwapa ujuzi wa kidijitali, huku familia zikihimizwa kufuatilia kile ambacho watoto wanatumia kwenye majukwaa ya kidijitali ili kuepuka maudhui yasiyofaa au upotoshaji wa taarifa. Kiliwataka wazazi na jamii kuwajali zaidi watoto wenye mahitaji maalumu na kuhakikisha wanajumuishwa katika mazingira ya kijamii yanayokubalika.

Miongoni mwa mapendekezo muhimu yalikuwa:

  • kukuza thamani za Kiislamu na ibada kwa watoto
  • kuandaa mkakati wa Kiislamu wa kitaifa kuhusu ustawi wa watoto na vyombo vya habari vya Kiislamu
  • kuingiza kanuni hizi katika sheria za kitaifa
  • kuandaa miongozo ya kielimu kwa watendaji wanaoshughulika na watoto
  • kuendeleza michezo ya mwili kupitia wakfu maalumu kwa watoto wenye mahitaji maalumu
  • na kuandaa warsha za kuelimisha wazazi wa Kiislamu kuhusu changamoto za sasa za malezi, kulinda utambulisho wa kidini na heshima ya asili ya mwanadamu.

Kuhusu kanuni ya istishab, Chuo hicho cha fiqhi kilithibitisha kwamba ni njia halali ya kisheria inayodumisha hali ya awali bila kutoa hukumu mpya, na inaweza kutumika kuthibitisha au kukanusha jambo kulingana na uhakika au shaka iliopo.

Kuhusu akili mnemba (AI), IIFA ilipendekeza uendelezaji wa utafiti kuhusu utambulisho wa kisheria wa AI, na kuitisha kongamano maalumu kuangazia maendeleo ya AI na masuala yake ya kimaadili.

Kuhusu malipo ya riba na dhamana, Chuo kiliahirisha maamuzi hadi uchunguzi zaidi ufanyike.

Kuhusu michezo ya kidijitali na kielektroniki, Chuo kilieleza kwamba ni shughuli shirikishi za kimwili na kiakili zinazofanyika kupitia teknolojia ya kisasa au majukwaa ya kidijitali kama vile michezo ya mapambano, majanga, mafumbo, na michezo ya mashindano. Kilitoa hukumu kwamba uchezaji wa michezo hiyo unaruhusiwa, mradi hauna ukiukaji wa kidini au kimaadili, na hauleti madhara kwa imani, akili, mwili, mali au mtu mwingine. Uzalishaji na biashara ya michezo hiyo na vibali vya malipo ya awali vya michezo (prepaid cards) pia vimeruhusiwa chini ya masharti hayo.

Chuo kilihimiza kuandaliwa kwa miongozo ya elimu ya kidijitali, kuwekwa kwa mifumo ya udhibiti kupunguza madhara ya michezo ya kidijitali, kampeni za kuhamasisha jamii juu ya faida na hasara zake, pamoja na kuhimiza wabunifu kuunda michezo mbadala yenye maadili na thamani za Kiislamu.

Kuhusu afya ya akili na uwezo wa kisheria, Chuo kiligawanya magonjwa ya kisaikolojia katika aina tatu kulingana na athari zake katika ufahamu, uelewa, na uwezo wa kufanya maamuzi, na kusisitiza kwamba tathmini za athari za ugonjwa wa akili katika uhalali wa kisheria zifanywe na wataalamu wa afya ya akili wenye sifa.

IIFA pia ilipendekeza programu za uelewa kwa mahakimu na wanazuoni kuhusu athari za kisheria za afya ya akili, pamoja na mafunzo ya pamoja kati ya wanasharia na wataalamu wa afya ya akili kuandaa miongozo ya kina.

Kuhusu masuala ya fedha, Chuo kilisisitiza maamuzi yaliyopita kuhusu umuhimu wa usimamizi wa kisheria wa Kiislamu katika benki za Kiislamu, ukiwemo wajibu, masharti, mbinu na uhuru wake, na kuhimiza mfumo wa pamoja wa kanuni ili kulinganisha uadilifu wa kidini na malengo ya kiuchumi katika taasisi za kifedha za Kiislamu.

Chuo pia kilitoa wito wa mfumo wa marejeo ya pamoja kwa sekta ya fedha ya Kiislamu, ili kulinda utambulisho wake na kuongoza maamuzi ya mikopo katika nchi wanachama na jamii za Kiislamu.

Kuhusu unyonyeshaji wa watoto njiti kwa maziwa yaliyotolewa na wengine, Chuo kilieleza kwamba unyonyeshaji ni mchakato wa maziwa ya mwanamke kufika tumboni mwa mtoto aliye chini ya umri wa miaka miwili, na kwamba watoto njiti wana haki ya kunyonyeshwa na mama zao au wachangiaji wengine wa maziwa. Wachangiaji hao wana haki ya kudumisha usiri wa utambulisho wao.

Chuo kilihimiza mamlaka za afya kuunda mifumo ya kisheria ya kudhibiti utoaji wa maziwa ili kulinda haki na ustawi wa kundi hili dhaifu, na kuzitaka wizara za afya kuhakikisha huduma bora na mikakati ya msaada kwao.

Kuhusu nyama zinazozalishwa kimaabara (lab-grown meat), Chuo kiliruhusu ulaji na uuzaji wake chini ya masharti maalum: seli zinazotumika lazima zitoke kwa wanyama wanaoruhusiwa kuliwa Kiislamu, wanyama hao lazima wawe wamechinjwa kwa mujibu wa sharia, na nyama hiyo isiwe imetengenezwa kwa kutumia vitu vilivyoharamishwa kama damu. Pia ilisisitizwa uwazi kamili kwa watumiaji, kufuata viwango vya usalama wa chakula, na kuhakikisha bidhaa hizi hazibadilishi nyama za asili.

Mwisho, kuhusu vyakula vilivyobadilishwa vinasaba (GM foods), Chuo kiliruhusu ulaji wake ikiwa vimechukuliwa kutoka kwa wanyama wanaoruhusiwa kuliwa, na mradi mchakato wake uko salama, unakubaliana na Sharia, na hauna madhara kiafya. Ilisisitiza umuhimu wa kutoa taarifa kamili kwa watumiaji kuhusu vyakula hivyo na jinsi vilivyoandaliwa.

3493003

captcha