IQNA

Mkutano wa OIC wapinga vikali pendekezo la kuhamishwa kwa nguvu Wapalestina wa Gaza

10:55 - March 09, 2025
Habari ID: 3480334
IQNA-Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imetoa taarifa rasmi mwishoni mwa kikao chake cha mjini Jeddah, Saudi Arabia na kulaani kwa nguvu zote njama za Marekani na Israel za kutaka kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina wa Ukanda wa Ghaza.

Mkutano wa dharura wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC ulifikia tamati usiku wa kuamkia Jumamosi mjini Jeddah, Saudi Arabia kwa kutolewa taarifa iliyoungwa mkono na washiriki wote wa mkutano huo. 

Katika taarifa hiyo, nchi wanachama wa OIC zimepinga vikali njama ya kulazimishwa kuhama Wapalestina na kusisitiza kuwa zinapinga kwa nguvu zote mpango huo.

Washiriki wa mkutano huo wamelaani vikali pia mashambulizi ya Israel dhidi ya Syria na uvamizi wake dhidi ya ardhi ya nchi hiyo ya Kiarabu na Kiislamu.

Taarifa hiyo pia imeidhinisha mpango wa Misri wa kujenga upya na kuboresha hali ya Gaza wakati wa awamu ya kwanza ya kurejea wakimbizi kwenye maeneo yao.

Wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu pia wametangaza kurejeshewa Syria uanachama wake katika jumuiya hiyo.

Kikao cha 20 cha dharura cha mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC ambacho ajenda yake ilikuwa ni "Uchokozi wa utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Palestina na njama za kulazimishwa Wapalestina kuondoka katika ardhi yao," kilifanyika jana Ijumaa, Machi 7, 2025 kwa pendekezo la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kikao hicho kimefanyika katika makao makuu yake ya mjini Jeddah, Saudi Arabia.

Mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu umefanyika ili kutoa msukumo na kuuhamasisha Ulimwengu wa Kiislamu kukabiliana barabara na njama zozote za kuwahamisha kwa nguvu wananchi wa Palestina kutoka Ukanda Gaza, ambazo bila shaka leo hii  zimeenea hadi Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, huku utawala wa Kizayuni pia ukiliweka katika ajenda yake ya kazi mchakato huu unaoongezeka wa kutaka kuwahamisha kwa nguvu wakazi wa Kipalestina wa Ukingo wa Magharibi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, aliyeshiriki katika kikao hicho cha Jeddah alisema Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) inapaswa kutoka kwenye maneno na kuchukua hatua za kweli, ikiwa ni pamoja  vikwazo vya pamoja dhidi ya Israel.  Huku akihimiza Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu kuzingatia misingi yake ya kuanzishwa, alisema "Mkutano huu lazima uwe hatua ya mabadiliko—si kwa maneno tu, bali kwa vitendo."

3492224

Habari zinazohusiana
captcha