IQNA

Ugaidi Afrika

Tawi la Al Qaeda ladai kushambulia kigaidi kambi ya kijeshi nchini Mali

18:19 - July 24, 2022
Habari ID: 3475532
TEHRAN (IQNA)- Washirika wa kundi la kigaidi la Al Qaeda nchini Mali wamedai kuhusika katika shambulio kwenye kambi kuu ya kijeshi ya nchi hiyo, ambayo wamesema ni jibu la ushirikiano wa serikali na washauri wa kijeshi kutoka Russia..

Uvamizi huo ulijiri Ijumaa kwenye kituo cha Kati kilichoko kilomita 15 nje ya mji mkuu Bamako na kupelekea mwanajeshi mmoja kuuawa na hiyo ilikuwa  mara ya kwanza katika uasi wa muongo mmoja wa Mali ambapo magaidi wakufurishaji wamelenga kambi ya kijeshi karibu na Bamako.

Uvamizi huo, uliotekelezwa na magaidi wakufurishaji kwa kutumia mabomu mawili ya kutegwa ndani ya gari, pia ulijeruhi watu sita, huku washambuliaji saba wakiuawa na wanane kukamatwa, jeshi la Mali lilisema.

Kitengo cha habari cha tawi la Mali la mtandao wa kigaidi wa al Qaeda, (JNIM), kilisema katika taarifa tawi lake la Katiba Macina lilifanya shambulio hilo.

3479825

Taarifa ya JNIM ilisema mpiganaji wa Mali alilipua bomu kwenye gari kwenye lango la kambi hiyo na mpiganaji kutoka Burkina Faso akalipua jingine ndani ya kambi hiyo, na kuruhusu wapiganaji wengine kuingia kambini.

Kundi hilo la kigaidi lilitetea  shambulio hilo na kusema limetekelezwa kupinga kuwepo nchini Mali washauri na askari binafsi wa Shirika Wagner la Russia. Shirika la Wagne  lilianza kusambaza mamia ya askari wake mwaka kote Mali kusaidia jeshi la Mali kukabiliana na makundi ya kigaidi baada ya jeshi la Ufaransa ambalo lilikuwa nchin humo kwa zaidi ya muongo moja kushindwa kuangamiza magaidi.

Serikali ya Russia imekiri kuwa wafanyikazi wa Wagner wako nchini Mali lakini serikali ya Mali imewataja kama wakufunzi kutoka Russia.

Katika taarifa tofauti siku ya Jumamosi, tawi hilo la kundi la kigaidi la Al Qaeda Mali lilidai kuhusika na mashambulizi katika miji mitano ya kati na kusini mwa Mali siku ya Alhamisi, ambayo jeshi la Mali lilisema lilimuua mwanajeshi mmoja na kujeruhi 15.

Kishikizo: mali magaidi al qaeda
captcha