IQNA

Usalama

Iran imewanasa magaidi 14 wa Daesh wakipanga njama za hujuma za kigaidi

13:56 - August 23, 2024
Habari ID: 3479314
IQNA-Wizara ya Usalama wa Taifa Iran imesema imewatia mbaroni magaidi 14 wa kundi la kigaidi la Daesh au ISIS, na hivyo kuzima njama zao za kutekeleza mashambulizi ya kigaidi ndani ya nchi.

Katika taarifa iliyotolewa siku ya Ijumaa, wizara hiyo ilisema baada ya msururu wa operesheni imefanikiwa kuwakamata magaidi 14 "wanaoongozwa na kundi la Kizayuni na Marekani la Daesh Khorasan (Daesh-K)" katika mikoa minne ya Iran ya Tehran, Alborz, Fars, na Khuzestan."

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, waliokamatwa waliingia katika Jamhuri ya Kiislamu kinyume cha sheria katika siku chache zilizopita kwa lengo la kufanya mashambulizi ya kigaidi.

Wizara hiyo pia ilisema kuwa magaidi saba kati ya hao walikamatwa mkoani Fars na wengine katika mikoa ya Tehran, Alborz na Khuzestan.

Wizara ya Usalama wa Taifa imebaini kuwa matokeo ya uchunguzi kamili yatachapishwa baadaye.

Ikumbukwe kuwa mnamo mwaka wa 2014, kundi la kigaidi la Daesh liliteka maeneo makubwa ya ardhi nchini Iraq na Syria na kuyatangaza maeneo waliyokuwa wakidhibiti kuwa ni "mamlaka ya ukhalifa."

Hata hivyo, vikosi vya Iraq na Syria, kwa msaada wa Iran, vilifanikiwa kushambulia ngome zote za Daesh na hatimaye nchi hizo mbili zilikombolewa  kutoka makucha ya kundi hilo la kigaidi miaka mitatu baadaye.

Bado, mabaki ya Daesh yanaendelea kufanya mashambulizi ya hapa na pale katika nchi tofauti.

Kundi hilo la kigaidi lilidai kuhusika na mashambulizi ya kigaidi katika mji wa Kerman kusini mashariki mwa Iran mnamo Januari 3, 2024 na kusababisha vifo vya watu 89 na kujeruhi wengine 284.

Kishikizo: iran magaidi daesh
captcha