IQNA

Hujuma za kigaidi zaendelea Afghasnitan, 33 wauawa Kunduz Afghanistan

15:23 - April 23, 2022
Habari ID: 3475157
TEHRAN (IQNA)- Idadi ya watu waliouawa shahidi katika shambulio la kigaidi lililotokea jana kwenye Msikiti mmoja wakati wa Sala ya Ijumaa huko Kunduz, kaskazini mwa Afghanistan wamefikia Waislamu 33.

Zabiullah Mujahid, msemaji wa serikali ya muda ya kundi la taliban huko Afghanistan amethibitisha shambulizi hilo la kigaidi na kusema kuwa watu 43 wamejeruhiwa katika mripuko huo. Kabla ya hapo, vyombo vya habari vya Afghanistan vilikuwa vimetangaza kuwa, watu waliouawa shahidi kwenye mripuko huo walikuwa ni 30.

Juzi Alkhamisi pia, gari lililokuwa limetegwa mabomu liliripuka karibu na Uwanja wa Ndege wa Kunduz mbele ya kituo cha upekuzi na kuua na kujeruhi watu wasiopungua 17.

Jumanne iliyopita pia, wanafunzi zaidi ya 27 waliuawa kufuatia shambulio la kigaidi katika shule moja ya wavulana katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul. Taarifa zilisema kuwa, magaidi waliokuwa wamesheheni mabomu waliishambulia Shule ya Abdul Rahim Shahid iliyopo katika mtaa wa Dashte Barchi ambao wakaazi wake wengi ni Waislamu wa madhehebu ya Kishia.

Ilidokezwa pia kuwa gaidi wa kwanza alijiripua  wakati wanafunzi walipokuwa wanaondoka shuleni baada ya kumalizika masomo ya asubuhi na baada ya muda usio mrefu gaidi wa pili akajiripua wakati walimu walipokuwa wakijaribu kuwasaidia waliokuwa wamejeruhiwa katika mripuko wa kwanza. 

Mashambulio ya kigaidi na miripuko kwenye maeneo tofauti ya Afghanistan inaonesha kuwa, serikai ya muda ya nchi hiyo imeshindwa kulinda usalama wa wananchi  na ndio maana makumi ya raia wasio na ulinzi wanauawa na kujeruhiwa mara kwa mara katika mashambulio ya kigaidi.

4051684

Kishikizo: afghanistan magaidi
captcha