NOUAKCHOTT (IQNA) - Gavana wa mkoa wa kusini wa Mauritania wa Gorgol alizindua usambazaji wa nakala 16,000 za Qur'ani Tukufu katika misikiti ya jimbo hilo.

Mpango huo ulizinduliwa katika hafla iliyofanyika katika mji mkuu wa mkoa hup mapema wiki hii, iliyohudhuriwa na maimamu, viongozi wa sala na wahubiri wa misikiti.
Gavana huyo alisema ni sehemu ya mpango wa kitaifa ambapo jumla ya nakala 300,000 za Kitabu Kitakatifu zitasambazwa misikitini, vituo vya kidini, vyumba vya maombi na vituo vingine nchini humo.
Alibainisha kwamba Misahafu hiyo imeandikwa katika mtindo wa Warsh na Qaloun kwa mujibu wa riwaya za Nafi.
Gavana huyo alisema Qur'ani Tukufu ni katiba ya Umma wa Kiislamu na kwamba Mauritania ambayo ni nchi yenye serikali ya Kiislamu inapaswa kuwa mstari wa mbele katika kukitangaza Kitabu hicho Kitakatifu.
Nakala hizo mpya zimechapishwa kwa amri ya rais wa Mauritania baada ya baadhi ya Misahafu inayotumika misikitini nchini humo kupatikana na makosa.
Nakala zenye makosa tayari zimekusanywa kutoka misikitini.
Kamati ya Qur'ani Tukufu ya Wizara ya Wakfu na masuala ya Kiislamu imesimamia uchapishaji na usambazaji wa nakala hizo mpya.
Mbinu za maandishi za Warsh na Qaloun kwa mujibu wa riaya ya Nafi ni hutumika kwa wingi katika nchi za Afrika Kaskazini na Magharibi, mbali na Misri. Jamhuri ya Kiislamu ya Mauritania ni nchi iliyoko katika eneo la Maghreb magharibi mwa Afrika Kaskazini.
Idadi ya watu nchini humo inakadiriwa kuwa takriban milioni 4 na takriban Wamauritania wote ni Waislamu. Shughuli na programu za Qur'ani ni maarufu sana katika nchi ya Kiafrika.