IQNA

Maimamu Watoharifu

Msomi: Imam Sadiq (AS) alihuisha mafundisho ya Kiislamu

18:24 - May 04, 2024
Habari ID: 3478766
IQNA – Mwanazuoni mwandamizi wa Kiislamu amesema Imam Sadiq (AS) alikuwa na nafasi muhimu katika kuhifadhi Uislamu na kuhuisha mafundisho ya Kiislamu kwa kuwafunza wanafunzi na kuiongoza jamii katika mwelekeo sahihi.

"Imam Sadiq (AS) alikuwa mwanzilishi wa fikra ambayo ilikuwa na jukumu muhimu katika kuhifadhi dini ya Uislamu na kuongoza jamii ya Kiislamu katika mwelekeo sahihi," Hujjatul-Islam Rahbar Mohammadi aliiambia IQNA siku ya Jumamosi.

"Shule yake ilikuwa na wanafunzi 4,000 waliobobea, ambao kila mmoja aliunga mkono hekima ya Imam na alijitahidi kuzuia kuenea kwa itikadi zilizo dhidi ya Uislamu na uharibifu miongoni mwa Waislamu," kasisi huyo aliongeza.

Kauli hiyo ilitolewa wakati Waislamu wa madhehebu ya Shia na wengineo nchini Iran na nchi nyinginezo leo Jumamosi wanakumbuka kufa shahidi Imam wa sita, Ima Sadiq (AS).

Siku kama ya leo miaka 1297 iliyopita Imam Ja'far Sadiq mmoja wa wajukuu wa Mtume Mtukufu (saw), aliuawa shahidi kwa amri ya mtawala dhalimu wa Kiabbasi Mansur al Dawaniqi. Imam Sadiq alizaliwa mwaka 83 Hijria katika mji mtakatifu wa Madina. Alishika hatamu za kuongoza Umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 31 baada ya kuuawa shahidi baba yake Imam Muhammad Baqir. Imam Sadiq ambaye kipindi cha uongozi wake kilisadifiana na zama za mapigano makali kati ya watawala wa Kiumawi na Kiabbasi, alitumia fursa hiyo kueneza elimu na maarifa sahihi ya Kiislamu.

Alifanikiwa kulea na kutayarisha wasomi hodari katika taaluma mbalimbali kama tiba, kemia, hesabati, nujumu hadithi na kadhalika. Jabiri bin Hayyan ambaye anatambuliwa hii leo kuwa ndiye baba wa elimu ya kemia alikuwa mwanafunzi wa Imam Ja'far Saqid (as). Ushawishi wa Imam ulienea kwa kasi katika ulimwengu wa Kiislamu, jambo ambalo halikuwafurahisha watawala wa Kiabbasi.

Hatimaye mtawala Mansur al Dawaniqi aliamuru Imam apewe sumu. Mtukufu huyo aliuawa shahidi kwa sumu hiyo katika siku kama ya leo na akazikwa katika makaburi ya Baqii mjini Madina.Alikuwa na maisha marefu zaidi miongoni mwa Maimamu wengine (AS) isipokuwa Imam Zaman (Mwenyezi Mungu aharakishe ujio wake). Hivyo, anaitwa pia Sheikh-ul-Aimma.

Hujjatul-Islam Rahbar Mohammadi  anasema Shule ya fikra iliyoanzishwa na Imam Sadiq (AS) ilitumika kama kinara kwa ajili ya kufufua mafundisho ya Kiislamu.

Mafanikio ya madhehebu ya Shia katika elimu ya dini yanaweza kuhusishwa na jihadi ya kitamaduni iliyoongozwa na Imam Sadiq (AS), amesema msomi  huyo na kuongeza:  "Aliwasilisha Uislamu na sheria zake kwa mtazamo wa Ahlul-Bayt (AS) na utamaduni wa Shia, ambao umekita mizizi katika mafundisho ya Mtume Muhammad (SAW) na Imam Ali (AS), kwa ulimwengu."

Moja ya kanuni muhimu za maisha ya Imam Sadiq (AS) ilikuwa ni kufafanua dhana ya Uimamu na kueneza itikadi za dini kwa mtazamo wa madhehebu ya Shia, ameema Hujjatul-Islam Mohammadi. "Imam Sadiq (AS) alichukua kila fursa kutetea Ushia, na kueneza mafundisho ya kweli ya Uislamu kwa kutumia hoja zenye nguvu na zenye kukubalika."

Kama babu zake watukufu, Imam Sadiq (AS) alijitahidi kuurekebisha Umma wa Mtume Muhammad (SAW) kutokana na mikengeuko na upotofu wowote, amebaini Hujjatul Islam Mohammadi, na kuongeza kwamba Imam Sadiq (AS) alikuwa bingwa na mfufuaji wa itikadi takasifu ya Shia na Uislamu sahihi.

Juhudi za Imamu Sadiq (AS) katika kufafanua fikra za madhehebu ya Shia, kuimarisha imani, kukuza maadili,  kuanzisha chuo kikuu, na kutoa mafunzo kwa wanafunzi wenye ujuzi ni sehemu ya michango yake ya kimsingi katika nyanja ya kitamaduni na kidini, Sheikh Mohammadi amebaini.

3488191

Kishikizo: Imam Sadiq
captcha