IQNA

Imam Sadiq AS alisisitiza umoja wa Waislamu

16:15 - June 17, 2020
Habari ID: 3472873
Siku kama ya leo miaka 1293 iliyopita Imam Ja'far Sadiq (AS) mmoja kati ya wajukuu wa Mtume Mtukufu Muhammad (SAW), aliuawa shahidi kwa amri ya mtawala dhalimu wa Kiabbasi, Mansur al Dawaniqi.

Tarehe 25 Shawwal mwaka 148 Hijiria, ulimwengu wa Kiislamu ulipatwa na huzuni kufuatia kuondokewa na mmoja wa Ahlul-Bayti wa Mtume wa Uislamu (saw). Katika siku hiyo, Imam Jafar Sadiq (as) akiwa na umri wa miaka 65 aliuawa shahidi kwa amri ya Mansur Dawaaniq, mtawala wa pili wa Bani Abbasi baada ya kupewa sumu. Katika kipindi chetu cha leo tutazungumzia namna imam huyo mtukufu alivyoamiliana na watu akiwa kama marjaa wa Waislamu kutoka makundi yenye fikra na itikadi tofauti katika zama zake. Basi endelea kuwa nasi hadi mwisho wa kipindi hiki.

Licha ya kwamba Ahlul-Bayti wa Mtume walikabiliwa na changamoto tofauti kisiasa na kijamii, lakini walijitahidi kuhakikisha wanainua bendera ya dini ya Kiislamu katika zama zao zote. Dakta Shahid Mutahhari, mwanafikra mashuhuri wa Iran anaandika kwa kusema: " Ahlul-Bayti hao walikuwa wakichunga maslahi ya Kiislamu na Waislamu kwa ujumla. Katika mazingira yote mepesi au magumu, viongozi hao walikuwa wakichunga vivyo hivyo maslahi ya Kiislamu. Aidha katika kila zama viongozi hao walikuwa wakiunda mrengo maalumu wa mapambano, huku wakiupatia elimu kamili mrengo huo ambao ulikuwa na jukumu la kulinda Uislamu." Moja ya sifa za kipekee za kipindi cha Imam Swadiq ilikuwa ni kuibuka makundi tofauti ya kiitikadi na kisiasa.

Mlinzi wa Uislamu

Suala hilo lilikifanya kipindi cha Uimamu wa mtukufu huyo kuwa kipindi muhimu zaidi kati ya vipindi vya maimamu wengine watoharifu katika historia ya Uislamu. Katika matukio yote hayo, Imam Swadiq (as) aliendelea kuulinda Uislamu kwa kuwalea maelfu ya wanafunzi wake kifikra na kitamaduni. Imam alisisitiza juu ya udharura wa kuenezwa mafundisho ya kidini sanjari na kukabiliana na bidaa na fikra zilizo kinyume na Uislamu. Katika harakati hizo, mtukufu huyo alikuwa akibainisha mafundisho na elimu ya Kiislamu kama vile hadithi, fiq'hi, aqida, tafsiri ya Qur'ani na elimu nyenginezo.

Aidha imam alikuwa akiyashawishi makundi mbalimbali ya Waislamu yaliyokuwa na mahusiano naye sambamba na kuwakurubisha karibu yake. Imepokelewa kuwa imam Jafar Swadiq (as) alikuwa na mahusiano mema na maulama wa Kisuni pia. Kwa mtazamo wa imam, farqa, ilikuwa ni chanzo cha kuibua mtetemeko katika ngome ya Uislamu. Ni kwa ajili hiyo ndio maana akawa akiwahusia Waislamu hususan wafuasi wake juu ya upendo baina yao wao kwa wao. Kuhusiana na suala hilo anasema: "Wafikishie salam wafuasi wetu na wambie kwamba Mwenyezi Mungu anamrehemu mtu ambaye anavutia kwake mapenzi ya watu." Mwisho wa kunukuu.

 

Umoja wa Waislamu

 

Aidha Imam Sadiq (as) alikuwa akiamini kwamba madhehebu na makundi tofauti ya Kiislamu, ni wahusika katika jamii ya Kiislamu na kwamba ni lazima kuheshimu fikra na mrengo wa mwengine.  Kwa ajili hiyo Waislamu mbali na kulinda mahusiano na urafiki kati yao, wanatakiwa pia kushirikiana kwa pamoja katika kutatua matatizo ya watu wengine. Hivyo ndivyo imam alivyokuwa akifanya na hivyo ndivyo alivyokuwa akiwahusia wafuasi wake.

Imepokelewa kuwa Waislamu wawili walihitilafiana baada ya kujiri mjadala baina yao. Sahaba mmoja wa imam aliyekuwa akifahamika kwa jina la Mufadh-dhal akapita eneo la tukio. Akiwa katika pitapita zake ndipo akafahamu kuwepo mjadala huo. Mufadh-Dhal akawachukua watu wale na kwenda nao nyumbani kwake na kuwambia:"Imam ameniamuru kwamba, popote pale nitakapoona tofauti kati ya Waislamu wawili, basi nirejesha amani na udugu baina yao, na hata kama ikilazimu basi niwagawie mali za imam. Hivyo chukueni hizi Dirham 400 ilimradi tu muweze kurejesha udugu wenu na muweke nguvu zenu pamoja."

Imam Jafar Sadiq ambaye ni moja ya wajukuu watukufu wa Mtume Muhammad (saw), hakufanya kitendo chochote ambacho kinaweza kuhesabiwa kuwa moja ya sababu za kuibua farqa au kitendo ambacho hakitakuwa na maslahi kwa makundi au madhehebu mengine ya Kiislamu. Kunasibiana na Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), elimu yake ya hali ya juu, akhlaqi njema na mambo mengine, ni miongoni mwa mambo yaliyokuwa yakiwavutia watu wengi na hivyo kumfanya mtukufu huyo kuwa kimbilio na marejeo ya watu na makundi mbalimbali wakati huo. Kama vile ilivyopokelewa kwamba, katika msimu wa ibada ya hija Imam Sadiq (as) alikuwa akikaa eneo la wazi kisha watu mbalimbali wakienda kando yake na kumuuliza maswali na yeye kuwajibu maswali yao.

Mahusiano na watu wa matabaka tafauti

Kukithiri watu waliokuwa wakienda kumtembelea mtukufu huyo, na mahusiano yake aliyokuwa nayo kwa matabaka ya watu tofauti, ni mamabo yaliyomtia wasi wasi mkubwa mtawala wa wakati huo, Mansur Dawaaniq. Abuhanifa ambaye ni mmoja wa viongozi wa Ahlusunna wal-Jamaa mbali na kumtaja Imam Sadiq (as) kuwa aliyekuwa mwenye elimu ya hali ya juu kati ya watu wote wa zama hizo anasimulia kisa cha kuvutia kumuhusu mtukufu huyo kuwa: "Siku moja Mansur aliniambia kwamba, watu wengi wamevutiwa sana na Imam Swadiq, hivyo andaa maswali magumu ili ufanye naye mjadala. Baada ya majlisi ya mjadala kuwadia, nilianza kumuuliza maswali yote huku Imam akiyajibu kwa kusema: nini mnaamini hivi, watu wa Madina wanaamini hivi na sisi tunaamini hivi. Katika baadhi ya mas'ala alikuwa akiafikiana nasi kama vile ambavyo alikuwa pia akiafikiana rai na watu wa Madina. Na sehemu nyingine alitofautiana na mirengo hiyo. Imam Swadiq alinijibu maswali yote 40 niliyokuwa nimeyaandaa ili kumshinda na kila swali alilijibu kwa mfumo huo. Je mtu anayefahamu tofauti za itikadi mbalimbali za watu si ndiye mtu mwenye elimu zaidi?"

 

Wanazunzi 4,000

 

Kati ya wanafunzi 4,000 wa mtukufu huyo, walikuwemo Ahlu Sunna, suala ambalo liliwafanya wasomi wa Ahlu Sunna kukubali marjaa ya kielimu ya Ahlu-Bayti wa Mtume (saw). Ni kwa ajili hiyo ndio maana katika mas'ala tofauti kama vile tafiri ya Qur'an na mengineyo, maulama hao wa Kisuni walikuwa wakienda kuuliza ufafanuzi wake kwa Imam Swadiq (as). Aidha imepokewa kuwa, makadhi wa Kisuni walikua wakimwendea mjukuu huyo wa Mtume na kumuuliza kuhusiana na mas'ala ya historian na kadhalika. Shakhsia kama Ma'adah bin Swadaqah ambaye alikuwa kadhi wa Kisuni, ni miongoni mwa makadhi maarufu waliofika kwa imam kuuliza masuala tofauti. Aidha Ahlul-Bayti wa Mtume walikuwa nao kwa upande mwingine  wakiwazuru watu hao na kuwatembelea sambamba na kutatua matatizo yao tofauti ya kielimu na kimada, na kumaliza kabisa mwanya wa mahusiano mema kati ya Masuni na Mashia, katika kipindi cha Imam Sadiq (as). Ni kwa ajili hiyo ndio maana Ahlul-Bayti wa Mtume (saw) wakahesabika katika jamii kuwa sawa na baba kwa watoto wake, katika juhudi zao za kuuepusha umma na hatari yoyote ya upotofu na bidaa.

Imam Abu Hanifa na Imam Malik

Aidha miongoni wa wanafunzi wa Kisuni waliokuwa wakisoma kwa mtukufu huyo, ni pamoja na Imam  Abu Hanifa mwenyewe (Nuuman bin Thabit) na Imam Malik bin Anas. Kuhusiana na Abu hanifa amenukuliwa akikiri kwa kusema:"Mimi nilikuwa mwanafunzi halisi wa Jafar bin Muhammad." Huku sehemu nyingine akisema:"Lau kama si miaka miwili niliyosoma kwa mtukufu huyo, basi ningeangamia." Mwisho wa kunukuu. Naye kwa upande wake Malik bin Anas ambaye ni kiongozi wa kundi la Maliki anasimulia kumuhusu Imam Sadiq kwa kusema:"Katika kipindi ambacho nilikuwa nikisoma kwa Jafar bin Muhammad nilimuona na hali kuu tatu, aidha alikuwa akisali, au alikuwa amefunga saumu au alikuwa akisoma Qur'an na kamwe sikuwahi kumuona akiwa hayuko katika hali ya udhu. Hakuna mtu yeyote aliyemfikia Jafar bin Muhammad katika elimu na uchaji Mungu ..." Pamoja na yote hayo na kutokana na chuki za maadui Imam Sadiq akauawa shahidi katika siku kama ya leo. Baada ya kuuawa shahidi, mwili wa mtukufu huyo ukazikwa katika makaburi ya Baqii mjini Madina.

captcha