IQNA

Shule za Jadi za Qur'ani za Moroko Zinadumisha Jukumu Muhimu katika Kufundisha Qur'ani, Sayansi za Kidini

18:36 - July 05, 2024
Habari ID: 3479071
IQNA - Shule za kijadi za Qur'ani Tukufu nchini Morocco ambazo zilianzia mamia ya miaka iliyopita zimedumisha jukumu lao muhimu kama vituo vya elimu ya kidini.

Shule za Qu'rani, zinazojulikana kwa jina la Maktaba, pia zina jukumu la kufundisha sayansi na shule za kisasa katika zama za sasa, kulingana na ripoti ya Al Jazeera. 

Ripoti hiyo inahusu sherehe za mahafali zilizofanyika hivi karibuni kwa wahifadhi wa kike wa Qur'ani wanaosoma katika mojawapo ya shule hizo, Shule ya Faqihiya iliyoko Taroudant, Mkoa wa Sous, kusini magharibi mwa Morocco.

Wakiwa wameshikilia vibao vyao ambavyo aya za Qur'ani zilikuwa zimeandikwa, wasichana hao walifurahi sana kujifunza Kitabu hicho Kitukufu.

Salwa Ayat Huda, mmoja wa wasichana 30 ambao wamehifadhi Qur'ani alisema amepata mafanikio hayo makubwa kutokana na juhudi za walimu wa shule hiyo na kutiwa moyo na kuungwa mkono na wazazi wake.

Shule ya Faqihiya ni mojawapo ya mamia ya vituo vya jadi vya Qur'ani vinavyowapa maisha mapya wasichana ambao wameshindwa kusoma katika shule zinazosimamiwa na serikali.


Watafiti wa Qur'ani watafanya Mkutano nchini Morocco
Nasser Ayat Bunasr, mkuu wa shule hiyo anasema wasichana hao sio tu kwamba wanajifunza Qur'ani Tukufu na mafundisho ya kidini, bali pia wanapewa mafunzo ya lugha za kigeni, upishi, ushonaji nguo na michezo.

Alisema wasichana wengi wanatarajia kuendelea na masomo, kuingia chuo kikuu na kupata digrii za elimu ya juu.

Shule hiyo ina mbinu maalum ya ufundishaji wa kuhifadhi Qur'ani na imekuwa na mafanikio makubwa kutokana na ufaulu mzuri wa wanafunzi wake katika mashindano ya Qur'ani kitaifa na kimataifa.

Ibrahim al-Fatemi, mwalimu wa shule hiyo, anasema njia hiyo inawavutia wanafunzi tangu awali, na kuwahimiza kufanya mazoezi na kujifunza aya za Quran kwa moyo.  


Washindi wa Shindano la Qur'ani la Morocco Watunukiwa
Kwa mujibu wa Mahdi bin Muhammad al-Saeedi, msomi wa chuo kikuu, shule za jadi za Qur'ani zilianza kuanzishwa nchini Morocco baada ya kuwasili Uislamu nchini humo.

Shule za kwanza zilianzishwa katika mji wa Fes na Almoravids au nasaba ya al-Murabitun na kisha shule zaidi za Qur'ani zilionekana katika maeneo mengine ya nchi, Munir Aqsabi, mtafiti wa Kiislamu anasema.

Alisema shule hizo zilianzishwa ili kufufua shule ya fikra ya Maliki na kutoa mafundisho ya Kiislamu, kutoa mafunzo kwa wahubiri, mahakimu na wasomi.

Kwa mujibu wa Aqsabi, ufundishaji wa sayansi ya Qur'ani, usomaji, Hadith, Fiqh na Sharia ya Kiislamu ulikuwa na nafasi kubwa katika shule hizo.

Moroko ni nchi ya Kiarabu ya Kaskazini mwa Afrika inayopakana na Bahari ya Atlantiki na Bahari ya Mediterania. Uislamu ndiyo dini kuu nchini Morocco, huku asilimia 99 hivi ya watu wakiufuata.

3488997

Kishikizo: qur'ani morocoo mahafali
captcha