IQNA

Msanii wa Morocco mwenye ulemavu aandika Qur'ani kwenye ngozi ya mbuzi

20:42 - May 16, 2025
Habari ID: 3480689
IQNA-Omar al-Hadi, mchoraji wa maandishi kaligrafia wa Morocco mwenye umri wa miaka 60, ameushinda ulemavu wa mwili wa maisha yake kwa kuandika aya zote za Qur'ani Tukufu yote kwenye ngozi ya mbuzi.

Akifanya kazi bila kuchoka kwenye chumba kidogo cha sanaa ndani ya nyumba yake huko Quneitra, kaskazini mwa Rabat, Omar amenakili aya za Qur'an kwa uangalifu mkubwa. Licha ya ulemavu wa mwili, anajitolea kikamilifu kwa kazi yake, akizungukwa na zana na vifaa vya maandishi.

Safari yake ilianza mwaka 2015, akichagua asubuhi ya Ijumaa kwa umuhimu wake wa kidini. Katika kipindi cha miaka mitatu, alitengeneza kwa uangalifu kila ukurasa, na kuweza kuandika kurasa 565 kwenye ngozi ya mbuzi, kila moja ikiwa na vipimo vya sentimita 55  kwa 36. Msahafu huu una uzito wa takribani kilo 100. Omar anaamini kazi yake ni ya kipekee na kuiita mafanikio katika  maandishi ya Qur'ani. Msahafu huu unajulikana kwa uzuri wa maandishi yake, na wanafunzi wachanga wanamsaidia kuhakikisha usahihi kwa kupitia kazi yake.

Vipaji vya Omar vinaenea zaidi ya kaligrafia na aaweza kufanya kazi kwa ustadi na mbao, ngozi, na shaba, akizalisha kazi za kuvutia. Akiungwa mkono na marafiki, alikumbatia changamoto ya kuandika Qur'ani, akiona kazi hii kama jitihada za sanaa na ibada. Mke wake anasimulia kujitolea kwake, akifanya kazi kuanzia saa 2 asubuhi hadi magharibi, akichukua mapumziko machache.

Msanii wa kujifunza mwenyewe tangu umri wa miaka saba, Omar amekuwa akifanya kazi hii ya kaligrafia kwa miaka 35 . Pia alianzisha shule za kufundisha watoto, akigeuza shauku yake kuwa dhamira ya maisha. Marafiki zake wa utotoni wanathamini kipaji chake, wakisisitiza ustahimilivu wake na uwezo wake wa kusoma Qur'an'. Bila kushindwa na ulemavu, Omar anaendelea na kazi yake, na anakusudia kuandika nakala nyingine ya Msahafu ambao anataka uwekwe ndani ya Msikiti Mkuu wa Makka.

3493097

Kishikizo: morocoo qurani tukufu
captcha