Washiriki wa mkutano wa Riyadh walitoa taarifa mwishoni mwa mazungumzo yao jana Jumatatu, ambapo walisisitiza juu ya kuunga mkono haki za watu wa Palestina, ikiwa ni pamoja na haki ya kuwa na uhuru na kuwa taifa huru na linalojitawala.
Taarifa hiyo ya kikao cha Riyadh imetilia mkazo haki ya wakimbizi wa Kipalestina kurejea makwao na kuwalipa fidia wakimbizi hao kama ilivyosisitizwa na maazimio husika ya kimataifa hususan azimio nambari 194 la Umoja wa Mataifa.
Katika taarifa hiyo imeelezwa pia kwamba: suala la Palestina ni kama yalivyo masuala mengine yote yanayohusu haki ziliyonayo mataifa ya kupambana ili kujikomboa na kuondokana na kuvamiwa na kukaliwa ardhi yao; na kwa hiyo uamuzi au hatua yoyote ya Israel ya kuiyahudisha Baitul Muqaddas (Jerusalem) Mashariki inayokaliwa kwa mabavu na kushadidisha ukaliaji wake haikubaliki.
Washiriki wa kikao cha Riyadh wamesisitiza pia kuhusu mamlaka kamili iliyonayo Serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina juu ya Quds ukiwa ndio mji mkuu wa milele wa Palestina.
Taarifa hiyo imeeleza pia kwamba: Quds Tukufu ni mstari mwekundu kwa Umma wa Kiarabu na Kiislamu na kuna ulazima wa kuonyesha mshikamano kamili wa kuunga mkono utambulisho wake wa Kiarabu na Kiislamu.
Mbali na taarifa ya Riyadh kusisitiza uungaji mkono kamili kwa Jamhuri ya Lebanon, usalama, uthabiti na mamlaka yake ya kujitawala pamoja na usalama wa raia wake; imetilia mkazo pia maazimio yaliyopitishwa katika mkutano uliopita na kukabiliana na hujuma za Israel dhidi ya Ghaza na Lebanon sambamba na kutolewa indhari kuhusu hatari ya kuongezeka mivutano katika eneo na kupanuka wigo wa uchokozi wa utawala huo wa Kizayuni ambao sasa hivi umeshasambaa hadi Lebanon.
Taarifa hiyo imelaani pia jinai za kutisha za jeshi la utawala wa Kizayuni na mauaji ya kimbari linayofanya huko Ghaza, ambapo mbali na hayo, washiriki wa kikao cha Riyadh wametaka kusitishwa mara moja mapigano nchini Lebanon na kutekelezwa kikamilifu azimio nambari 1701, na kutahadharisha juu ya hatari ya kukiukwa mamlaka ya kujitawala ya Syria na Iran kutokana na upuuzaji wa jamii ya kimataifa na taasisi za kimataifa.
Taarifa ya mwisho ya kikao cha Riyadh imesisitizia pia udharura wa Baraza la Usalama la UN kupitisha azimio lenye ulazima wa utekelezaji kwa mujibu wa Sura ya Saba ili kuulazimisha utawala wa Kizayuni utekeleze usitishaji vita huko Ghaza na kulitaka pia baraza hilo liitikie wito unaotolewa kwa kauli moja kimataifa kwamba Palestina inastahiki kuwa mwanachama kamili wa Umoja wa Mataifa.
Aidha, taarifa ya kikao cha Riyadh imezitaka nchi zote zisiipelekee silaha na zana za kivita Israel, na kulitaka pia Baraza la Usalama lichukue maamuzi yanayohitajika ili kusimamisha hatua za kinyume cha sheria na za kuzusha mivutano za utawala wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi.
Kikao cha pili cha dharura na cha pamoja cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kilifanyika jana Jumatatu huko Riyadh, mji mkuu wa Saudi Arabia, kwa kuhudhuriwa na viongozi wa zaidi ya nchi 50.
Kikao hicho kilifanyika kwa pendekezo la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na ufuatiliaji wa waziri wake wa mambo ya nje Sayyid Abbas Araghchi.
3490655