IQNA

Mkutano wa Makka waafiki jitihada za umoja wa madhehebu za Kiislamu

19:03 - March 10, 2025
Habari ID: 3480344
IQNA – Wanazuoni wa Kiislamu kutoka sehemu mbalimbali za ulimwengu wa Kiislamu waliokutana katika mji mtakatifu wa Makka wamefikia muafaka  kuhusu Ensiklopidia ya Makubaliano ya Kifikra ya Kiislamu pamoja na Mpango wa Mkakati wa kuimarisha Umoja kati ya Madhehebu za Kiislamu.

Hati hizi zilikubaliwa mwishoni mwa toleo la pili la mkutano wa kimataifa wa 'Kujenga Madaraja Kati ya Madhehebu ya Kiislamu', ulioandaliwa mjini Makka tarehe 6-7 Machi.

Mkutano huo uliwaleta pamoja wawakilishi wa madhehebu na fikra za Kiislamu kutoka zaidi ya nchi 90 chini ya kaulimbiu "Kuelekea Ushirikiano Madhubuti wa Kiislamu."

Washiriki pia walishuhudia uzinduzi wa Ensiklopidia ya Makubaliano ya Kifikra ya Kiislamu, ambayo inasimamiwa na Kituo cha Kulinda Fikra cha Wizara ya Ulinzi ya Saudi Arabia, na imeandaliwa na wanazuoni sitini.

Ensiklopidia hiyo ilipitiwa na Sekretarieti Kuu ya Baraza la Wanazuoni Wakuu wa Saudi Arabia, pamoja na wajumbe wa Akademia ya Fiqhi ya Kiislamu na Baraza Kuu la Jumuiya ya Kiislamu Duniani (MWL), ili kutoa mfumo wa mwongozo kwa mahusiano baina ya madhehebu kwa misingi ya maadili ya Kiislamu yanayowaleta pamoja Waislamu wote.

Mkutano huo ulisifu juhudi za Jumuiya ya Kiislamu Duniani (MWL) katika kufafanua upya mahusiano ya kimadhehebu kupitia Hati ya Kujenga Madaraja, kuhakikisha kuwa juhudi hizo si nara tupu bali zinaimarishwa kwa programu za kivitendo na ushirikiano wa kimkakati kwa lengo la kuleta mshikamano na umoja ndani ya ulimwengu wa Kiislamu.  Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliwakilishwa katika kikao hicho na Hujjatul Hamid Shahriyari Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu.

3492248

captcha