Sheikh Abaei, mmoja wa watu wanaoheshimika sana katika nyanja ya Qur’ani nchini Iran, alifariki dunia tarehe 9 Aprili 2025 akiwa na umri wa miaka 80, baada ya maisha ya kujitolea kwa ajili ya kuhudumia na kueneza Qur’ani Tukufu.
Alihudumu kama jaji katika mashindano ya kitaifa na ya kimataifa ya Qur’ani kuanzia mwaka 1985 hadi 2018, alipoamua kujiondoa kutokana na maradhi.
Katika salamu za rambirambi katika nyakati tofauti, mashekhe wa Qur’ani kutoka Misri akiwemo Sheikh Abdul Fattah al-Taruti, Sheikh Ahmad Farajullah Shazli, Sheikh Taha Mohamed Abdul Wahab, Sheikh Mohamed Ali Jabin, na Sheikh Abdullah Abdullah walitoa pole kwa watu wa Iran, jamii ya Qur’ani ya Iran, na familia ya marehemu huyu mwanaharakati wa Qur’ani.
Katika ujumbe wake, Sheikh Shazli aliandika: “Mwalimu mpendwa Abdolrasoul Abaei alikuwa mtu mwenye huruma na baba mwenye upole. Ulipokutana naye kwa mara ya kwanza, ulikuwa na hisia kama unamfahamu kwa muda mrefu. Nilimwona kuwa mtu mwema, mkarimu, mwenye moyo wazi, mwenye nuru, hekima, uaminifu, na kipenzi cha wengi. Roho yake ilikuwa nyepesi na ilikubalika kwa wengi. Mbali na elimu yake kuhusu sanaa ya tilawa ya Qur’ani, matamshi, na ufuataji wa kanuni za tajwidi, alihesabiwa kuwa miongoni mwa mashekhe wa heshima ambao mfano wao ni adimu kuonekana. Kutokuwepo kwake ni pengo lisilozibika, na ni nadra kuwepo tena mtu mfano wa Ustadh Abaei, ambaye pia alikuwa profesa wa fasihi na mtu wa maadili ya hali ya juu. Nawapa pole watu wa taifa la Kiislamu la Iran kwa msiba huu, na namuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu amsamehe marehemu, amrehemu kwa mapana, na atupatie sisi sote subira na malipo makubwa.”
Naye Sheikh Taruti katika ujumbe wake alimtaja marehemu Abaei kama: “Mwalimu mashuhuri na rafiki wa dhati.”
Aliandika: “Kwa niaba ya jumuiya nzima ya Qur’ani hapa Misri, nawapa rambirambi za dhati watu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa kumpoteza kipenzi chetu, Mwalimu Abdolrasoul Abaei (rahimahu Allah). Abaei alikuwa mwalimu wetu, mpendwa katika nyoyo zetu, na tulishiriki naye kumbukumbu nyingi nzuri katika majukwaa kama mahakimu wa mashindano ya Qur’ani na mikutano ya Qur’ani. Marehemu Abaei alikuwa baba bora, mwalimu mahiri, na rafiki wa dhati. Namuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu amrehemu kwa huduma zake kwa Qur’ani na watu wake, amkubali kuwa miongoni mwa walioongoka, na aipe familia yake malipo mema, atupe sisi nguvu ya moyo, na amuweke marehemu miongoni mwa watu wa Peponi.”
Sheikh Jabin kwa upande wake amesisitiza jinsi Mwalimu Abaei alivyojitolea maisha yake kwa Qur’ani, akisema:
"Mwanazuoni mkubwa wa Qur’ani na mtu aliyetoa maisha yake kwa ajili ya kutumikia Kitabu cha Mwenyezi Mungu katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na ulimwengu wa Kiislamu, Qari mashuhuri Mwalimu Abdolrasoul Abaei, amefariki dunia."
Akaongeza: "Tunatoa rambirambi zetu kwa familia ya Qur’ani. Kupotea kwa qari ni hasara kubwa sana, hasa kwa kuzingatia athari ambayo Mwalimu Abaei aliacha kwa vizazi vya waqari waliokuja baada yake ndani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran."
Sheikh Abdul Wahab naye alielezea rambirambi zake za dhati kuhusu kifo cha Mwalimu Abaei:
"Ummah wa Kiislamu umepoteza mmoja wa wanazuoni wake muhimu kabisa katika nyanja ya tafakuri ya Qur’ani, mwanazuoni mwenye heshima Abdolrasoul Abaei (rahimahu Allah). Nawapa rambirambi zangu za dhati marafiki wote na majaji wa kimataifa waliopata kumfahamu marehemu katika mashindano ya kimataifa, na waliomuona kama baba, ndugu, na mwalimu, ambaye kutoka kwake tulijifunza mbinu mbalimbali za kuhukumu na adabu."
"Pia nawapa pole wote wanaompenda na kumuenzi mwanazuoni huyu mkubwa. Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu ampe makazi miongoni mwa manabii, wakweli, na mashahidi. Na Qur’ani Tukufu, ambayo aliitumikia maisha yake yote, iwe ni yenye kumtetea mbele ya Mola Siku ya Qiyama – kwa ajili yake na kwa ajili yetu sote."
Ujumbe wa rambirambi kutoka kwa Sheikh Abdullah Abdullah ulikuwa huu:
"Katika wakati huu mgumu na wenye maumivu, tunatoa pole zetu kwetu wenyewe na kwa jamii ya Qur’ani kufuatia kufariki kwa mwanazuoni, mfasihi, na msomaji mwaminifu, Mwalimu mkubwa wa Qur’ani kutoka Iran, Abdolrasoul Abaei (rahimahu Allah)."
"Ujumbe huu wa rambirambi si maneno tu, bali ni mwangwi wa hisia na heshima kwa historia tukufu ambayo imekuwa mwangaza kwa njia ya jamii ya Qur’ani nchini Iran na ulimwengu wa Kiislamu. Mwalimu Abaei alikuwa mfano wa kujitolea na ukarimu katika kuutumikia Kitabu cha Mwenyezi Mungu, na kueneza maana yake tukufu kwa wote waliotafuta kukaribia nuru ya Qur’ani."
"Kupotea kwake ni jeraha kubwa ndani ya moyo wa Ummah wa Kiislamu, kwani alikuwa mtu aliyekuwa akiongoza daima, akisaidia wenye mapenzi kwa Qur’ani, akipanda mbegu za hekima na uongofu kila mahali, na kuacha athari ya kudumu ndani ya nafsi za watu, pamoja na kutoa matumaini angavu kwa vizazi vijavyo vyote."
4276159