IQNA

Hati ya Kitabu cha Ibn Sina yaonyesha uhusiano wa madaktari wa Kiarishi na Ulimwengu wa Kiislamu

23:15 - April 19, 2025
Habari ID: 3480565
IQNA – Ugunduzi wa hati ya kale ya Kiarishi umeonyesha uhusiano usiotarajiwa kati ya utamaduni wa Gaelic huko Ireland na ulimwengu wa Kiislamu. 

Kwa mujibu wa ripoti ya Al Jazeera, kipande kidogo cha ngozi, sehemu ya hati ya Kiarishi ya enzi za kati na sehemu ya kitabu kilichotumika kati ya miaka 1534 na 1536 Miladia (CE) kama mwongozo wa Kilatini kwa serikali ya eneo la London, kimegunduliwa hivi karibuni. 

Kitabu hiki kilikuwa katika umiliki wa familia ya Kiingereza huko Cornwall, ambayo kwa kushangaza imekihifadhi kama urithi wa familia hadi leo. 

Hati hii ni sehemu ndogo ya kitabu cha  "Canon of Medicine" (al-Qānūn fī al-tibb) yaani Kanuni ya Tiba kilichoandikwa na mwanasayansi wa Kiajemi Ibn Sina (Avicenna). Nakala hiyo iliyopatika imefsiriwa kwa lugha ya Kiarishi. 

Kitabu cha Ibn Sina kilikuwa marejeo muhimu ya taaluma ya  matibabu katika Ulaya ya enzi za kati na kilitafsiriwa kwa lugha mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Kilatini na Kiingereza. 

Karne moja baada ya kitabu kuchapishwa, sehemu ya hati asilia, ambayo ilitumika kufunga na kupamba jalada na kingo zake, iligunduliwa na Profesa Pádraig Ó Macháin kutoka idara ya Masomo ya Kiarishi katika Chuo Kikuu cha Cork, mtaalamu maarufu katika uwanja wake, ambaye alivutiwa sana na hati hiyo. 

Macháin anaamini kuwa madaktari wa Kiarishi walinufaika na maarifa ya matibabu kutoka Mashariki ya Kati na Iran karne nyingi zilizopita.

Ugunduzi wake pia ulithibitisha kuwa kitabu maarufu "Canon of Medicine" cha Ibn Sina kilitumika katika Ireland ya enzi za kati kufundisha madaktari wapya. 

Gaelic ni lugha ya kitaifa na kihistoria ya watu wa Ireland na inazungumzwa kama mojawapo ya lugha mbili rasmi za nchi hiyo pamoja na Kiingereza.

Kitabu cha Ibn Sina cha matibabu kinachukuliwa kuwa kitabu kikuu cha matibabu duniani na kina sehemu tano.Kilikuwa kimeandikwa na Ibn Sina mnamo mwaka 1025 Miladia (CE). Kitabu kinaonyesha maarifa ya matibabu katika ulimwengu wa Kiislamu lakini pia kimeathiriwa na matibabu ya Kiajemi, Kiyunani-Kirumi, na Kihindi. 

Hati iliyogunduliwa hivi karibuni ina sehemu kutoka sura za mwanzo kuhusu fiziolojia ya taya, pua, na koo. 

Kutokana na umuhimu wa ugunduzi huu katika historia ya elimu ya matibabu Ireland, wapenzi wa "Canon of Medicine" wamekubaliana kuchapisha hati hii na kuifanya ipatikane kidigitali kwa umma. 

Ibn Sina mwanafalsafa na tabibu mashuhuri wa Kiislamu na Kiirani aliyejulikana pia kwa laqabu ya Sheikhul Rais alizaliwa tarehe 3 Safar mwaka 370 Hijria Qamaria katika mji wa Balkh. Ibn Sina alihifadhi Qur'ani yote alipokuwa na umri wa miaka 10. Msomi na tatibu huyo mashuhuri wa Kiislamu alijifunza tiba baada ya kupata elimu za mantiki, hisabati, nujumu, falsafa pamoja na elimu nyinginezo. Alianza kuandika vitabu akiwa na umri wa miaka 21 na miongoni mwa vitabu vyake maarufu ni Qanun, Shifaa na Isharaat.

3492735

Kishikizo: ibn sina
captcha