IQNA

Hija katika Qur’ani /3

Sa’i kati ya Safa na Marwa: Ibada ya Kitauhidi katika muktadha wa historia

10:28 - May 26, 2025
Habari ID: 3480740
IQNA – Safa na Marwa si milima miwili tu iliyopo karibu karibu na Msikiti Mtakatifu wa Makka. Ni alama za ibada, za Tauhidi, na kujitolea. Sa’i, yaani kitendo cha kutembea au kukimbia baina ya milima hiyo miwili, ambacho Qur’ani imekitaja kuwa miongoni mwa Sha’a’ir Allah (alama za ibada za Mwenyezi Mungu), ni kitendo chenye uzito kinachorejea katika tukio la kihistoria.

Kwa mujibu wa tafsiri za Qur’ani, neno Sha’a’ir ni wingi wa Sha’ira, na linamaanisha alama au nembo zilizowekwa mahsusi kwa ajili ya kutekeleza ibada. Sha’a’ir Allah ni alama ambazo Mwenyezi Mungu ameziweka ili waja Wake wamtumikie kwa unyenyekevu. Miongoni mwa hizo alama ni Safa na Marwa ; milima miwili ambayo leo hii ni njia zilizofunikwa karibu na Msikiti wa Haram, na mahujaji wanaamrishwa kuzipitia mara saba kwa kutembea au kukimbia.

Sa’i hii (kutembea kati ya milima hiyo miwili) ni ukumbusho wa kujitolea na unyenyekevu wa Bibi Hajar, mke wa Nabii Ibrahim (AS), aliyepita njia hiyo mara saba kwa imani thabiti kwa Mwenyezi Mungu (Tawakkul), akitafuta maji kwa ajili ya mwanawe Ismail. Kitendo hiki ni cha hali ya juu kabisa kwa mujibu wa Tauhidi (kumpwekesha Mwenyezi Mungu), kiasi kwamba Imamu Swadiq (AS) alisema: "Hakuna mahali bora duniani kuliko sehemu kati ya milima hiyo miwili."

Hii ni kwa sababu kila mwenye kiburi analazimika kuonyesha utiifu wake kwa Mwenyezi Mungu, akitembea au akikimbia kwa hali ya unyenyekevu, akiwa amevaa ihram, bila chembe ya majivuno.

Lakini katika Zama za Ujahiliya, sura ya ibada hii ilipotoshwa. Washirikina waliweka masanamu mawili - Usaf na Naila - juu ya milima hiyo, na walikuwa wakiyasujudia wakati wa kufanya Sa’i. Hali hii iliwapelekea baadhi ya Waislamu kufikiria kuwa Sa’i kati ya Safa na Marwa ni kitendo cha kijahili na kisichokubalika.

Ili kusahihisha dhana hiyo potofu, Qur’ani Tukufu ikabainisha wazi katika aya ya 158 ya Surah Al-Baqarah:

“Hakika vilima vya Safaa na Marwa ni katika alama za Mwenyezi Mungu. Basi anaye hiji kwenye Nyumba hiyo au akafanya Umra, si kosa kwake kuvizunguka. Na anaye jitendea mwenyewe kheri basi bila ya shaka Mwenyezi Mungu ni Mwenye shukrani na Mjuzi.”

Aya hii haikubainisha tu uhalali na utukufu wa maeneo hayo mawili, bali pia ilionesha kuwa kwa mujibu wa Qur’ani, alama za ibada hazifai kuachwa au kudharauliwa kwa sababu ya historia yao kuchafuliwa. Alama za Mwenyezi Mungu, hata zikiambatana na shirki au ujinga wa kihistoria, husafishwa na kurejeshwa katika hali yake ya asili kupitia nuru ya ufunuo au Wahyi na Tauhidi.

3493232

Kishikizo: hija qurani tukufu
captcha