Seyed Mehdi Sheikholeslami, ambaye ni miongoni mwa wajumbe wa “Msafara wa Nur” kutoka Iran, aliyasema hayo katika mahojiano maalum na IQNA akiwa mjini Makka.
Amesema kwamba pamoja na kutekeleza jukumu walilopewa kama wajumbe wa msafara huo, safari hii ya kiroho pia inawapa nafasi ya kuwasiliana na wasomaji wa Qur'ani kutoka mataifa mengine ya Kiislamu.
Akitilia mkazo umuhimu wa kutoa sauti ya pamoja dhidi ya uhalifu unaoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni nchini Palestina na Gaza, alisema: “Lugha ya pamoja miongoni mwa waliohudhuria Hija ni Qur'ani. Hivyo basi, kupitia usomaji wa aya zinazoangazia dhuluma, uonevu na kutetea wanyonge, wasomaji wa Qur'ani wanaweza kutimiza wajibu wao wa kibinadamu na kupaza sauti ya haki.”
Akaongeza kuwa mazingira ya usomaji wa Qur'ani katika kipindi cha Hija ni tofauti kabisa na yale ya mizunguko ya kawaida ya kisomo cha Qur'ani.
“Tofauti hii inatokana na unyeti na hali ya kiroho ya Hija, jambo ambalo huwapa wasomaji vijana wa Qur'ani tajriba ya kipekee na ya kiroho,” alisema Sheikholeslami, ambaye ana umri wa miaka 21 na ndiye mshiriki mdogo zaidi katika msafara huo wa Qur'ani.
Akaendelea kusema: “Nimefurahi sana kupata nafasi hii ya kuwa sehemu ya msafara huu mtukufu na kusafiri hadi katika Ardhi ya Wahyi nikiwa pamoja na maqari maarufu na wenye uzoefu mkubwa duniani. Nimejitahidi kujifunza zaidi kadri ya uwezo wangu huku nikitekeleza jukumu nililopewa.”
Kila mwaka, mamilioni ya Waislamu kutoka kote duniani husafiri kuelekea Makka, Saudi Arabia, kwa ajili ya ibada ya Hija. Iran pia hupeleka kundi la wanaharakati wa Qur'ani kuwa sehemu ya misafara ya Mahujaji wake.
Msafara wa Qur'ani wa Iran kwa ajili ya Hija, unaofahamika kama Msafara wa Nuru, ni sehemu ya juhudi za Iran kuboresha uzoefu wa kidini wa Mahujaji wake kwa kuandaa program mbalimbali zinazohusiana na Qur'ani wakati wa ibada ya Hija.
3493288