Katika aya ya 28 ya Surah Al-Hajj, Allah Subhanahu wa Ta‘ala anasema:
“…ili washuhudie manufaa yao, na walitaje jina la Mwenyezi Mungu katika siku zilizoainishwa...”
Aya hii inabainisha wazi lengo tukufu la Hija. Lengo hilo lina mwelekeo wa ibada na pia lisilo la ibada; yaani kumkumbuka Allah (SWT) na vilevile kunufaika na manufaa mbalimbali.
Kwa mujibu wa aya hii tukufu, watu wanaitwa katika Nyumba ya Mwenyezi Mungu ili washuhudie manufaa yao , manufaa ambayo, kwa mujibu wa Imam Ridha (AS), yanajumuisha watu wote wa ardhi hii, wawe wamehudhuria Hija au la.
Manufaa haya yameelezewa kwa namna ya jumla na hayajafungiwa upande wowote maalum. Wafasiri kama Ibn Abbas wameyachukulia haya kuwa ni manufaa ya kimwili na kibiashara, kwa mujibu wa aya nyingine katika Surah Al-Baqarah, aya ya 198:
“Si vibaya kwenu kutafuta fadhila kutoka kwa Mola wenu...”
Wengine wameyatizama manufaa haya kuwa ya kiroho pekee. Lakini ukweli ni kwamba, Hija hujumlisha manufaa yote , yawe ya kidunia au ya Akhera. Yakiwemo baraka za kiroho, matokeo ya kimwili, faida kwa mtu binafsi na kwa jamii, pamoja na falsafa za kisiasa, kiuchumi, na kimaadili.
Msingi wa mtazamo huu ni lugha ya aya yenyewe , iliyo huru na isiyo na mipaka ya kidunia au kiakhera.
Msimu huu mtukufu wa Hija huweza kuwa kitovu cha kuamsha nafsi za waumini wanaokandamizwa au wanaokumbwa na shida. Katika safari hii takatifu, Waislamu si tu kwamba huonesha umoja wa Kiislamu, bali pia huwasiliana, kushirikiana, na kupata habari za hali halisi ya Waislamu wa mataifa mbalimbali.
Zaidi ya hayo, tangazo la Bara’ah mina-l-mushrikiin (kujiweka mbali au kujibari washirikina), ambalo hufanywa wakati wa ibada ya Hija, limejengeka juu ya aya ya 3 ya Surah At-Tawbah:
“*Na ni tangazo kutokana na Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa wote siku ya Hija Kubwa kwamba Mwenyezi Mungu na Mtume wake hawana jukumu lolote kwa washirikina…”
Hili linaonesha wazi kipengele cha kisiasa cha Hija, na linaweza kutumika kama jukwaa la kutangaza sera kuu za Ummah wa Kiislamu.
Kwa muhtasari, Hija ni ibada yenye kuleta utakaso wa roho kwa dhikri ya Mwenyezi Mungu, nuru ya akili kwa mafunzo yanayopatikana, nguvu ya mwili kupitia nidhamu ya ibada, na mshikamano wa jamii kupitia umoja, uelewa, na kutambua maadui wake.
3493274