Wizara ya Masuala ya Kiislamu, Dawah na Mwongozo ya Saudi Arabia ilianza kusambaza nakala hizo za Qur'ani Jumapili, siku ya pili ya Tashreeq, kipindi cha ibada kinachofuata Idul Adha. Juhudi hizi zinawalenga Mahujaji wanaosafiri kwa njia ya ardhi, bahari, na anga.
Jumla ya nakala 2,521,380 zimetengwa kwa ajili ya usambazaji wa mwaka huu, kwa mujibu wa Shirika la Habari la Saudi (SPA).
Nakala hizo za Qur'ani ,zilizochapishwa katika ukubwa na lugha tofauti, zilitolewa na Kituo cha Mfalme Fahd cha Uchapishaji wa Qur'ani Tukufu kilichopo Madina.
Kwa mujibu wa SPA, “Nakala hizi ni zawadi kutoka kwa Mfalme Salman bin Abdulaziz Al Saud, Mlinzi wa Misikiti Miwili Mitakatifu.” Nakala hizo za Qur'ani hizo zinatolewa katika vituo vikuu vya kuondoka, ikiwemo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa King Abdulaziz, Bandari ya Kiislamu ya Jeddah, na vituo vya mpakani.
Hajj ni ibada ya kila mwaka inayofanyika Makka, ambayo kila Muislamu mwenye uwezo wa kimwili na kifedha anatakiwa kuitekeleza angalau mara moja katika maisha yake. Hija ya mwaka 2025 hivi karibuni imehitimishwa kwa ushiriki wa Mahujaji zaidi ya milioni 1.6 kutoka duniani kote.
Baada ya kukamilisha ibada kuu za Hija, mahujaji wengi sasa wanarejea katika nchi zao, huku wengine wakihitimisha safari yao ya kiroho kwa kutembelea Madina, ambako Mtume Muhammad (SAW) amezikwa.
3493395