IQNA

Hija Katika Qur’ani /4

Ibada ambayo inadhihirisha uchaMungu wa kina

13:04 - May 28, 2025
Habari ID: 3480751
IQNA – Kuheshimu alama za ibada za Mwenyezi Mungu ni ishara ya usafi wa ndani wa nafsi na moyo wenye kumcha Mwenyezi Mungu.

Yeyote ambaye ana uchaMungu wa kweli ndani ya moyo wake, atakuwa mnyenyekevu na mwenye heshima mbele ya Sha’a’ir Allah (alama za Mwenyezi Mungu).

Neno Sha’a’ir ni wingi wa Sha’ira, na linarejelea alama au ishara zilizowekwa kwa ajili ya kutekeleza ibada maalum.

Mwenyezi Mungu anasema katika Qur’ani Tukufu:
“Ndio hivyo! Na anayetukuza alama Mwenyezi Mungu, basi hayo ni katika unyenyekevu wa nyoyo. (Surat Al-Hajj, aya ya 32)

Katika aya hii, dhomir (zamir) "fa-innahā" (kwa hakika hiyo) inarejelea kuheshimu Sha’a’ir, maana yake ni kuwa heshima hii kwa alama za Mwenyezi Mungu inatokana na uchamungu wa moyo. Kwa maneno mengine, kuna uhusiano wa kina kati ya moyo wa mwanadamu na kuonesha heshima ya nje kwa hizi Sha’a’ir.

Kuambatanisha neno "taqwa" (uchamungu) na "qulub" (mioyo au nyoyo) pia kunaonesha kuwa chanzo halisi cha uchaMungu ni nafsi safi na nia njema, si maneno ya nje wala mienendo ya udanganyifu. UchaMungu wa maneno pekee au vitendo vya kujionesha bila mizizi ya moyo ni unafiki, na hauna thamani ya kweli mbele ya Mwenyezi Mungu.

Tafsiri ya Qur’ani ya Ruh al-Ma’ani inasisitiza kwamba neno “min” (kutoka) katika aya hii linaweza kuonesha sababu au mwanzo wa jambo. Katika hali zote mbili, maana yake ni kuwa kuheshimu Sha’a’ir kunatokana na uchaMungu wa moyo, au kunafanywa ili kufikia hali hiyo ya uchaMungu. Al-Imam Fakhr al-Din al-Razi naye ameieleza Sha’a’ir kama alama zinazobeba maana ya mambo ya Kimungu, ambazo hazipaswi kupuuzwa bali zinapaswa kukaribiwa kwa shauku na moyo mkunjufu, kwa kuitikia wito wa Mwenyezi Mungu bila kusita.

Aya hii inatoa mafundisho kadhaa muhimu:

  • Uchamungu wa ndani ni lazima uonekane katika tabia na ibada za nje;

  • Kupuuza Sha’a’ir ni dalili ya udhaifu wa uchaMungu wa moyo;

  • Kuheshimu alama hizi kunapaswa kutoka katika ikhlasi na uadilifu, si mashindano au unafiki;

  • Na hatimaye, ni moyo wa mwanadamu ndio kipimo na mahali pa hukumu mbele ya Mola Mtukufu.

3493252

Kishikizo: qurani tukufu hija
captcha