Kadhalika, aya nyingine zinabeba maana na ukweli ambao dhihirisho lake la wazi linajitokeza kwa namna ya kipekee katika kuashiria nafsi tukufu ya Imam Hussein (AS).
Mapambano ya Imam Hussein (AS) dhidi ya utawala wa Yazid bin Muawiya yalikuwa tukio la kihistoria, la kishujaa na la kiadilifu, ambalo limetukuka milele katika historia ya Uislamu. Imam Hussein (AS), aliyeasisi mapinduzi haya makubwa, alizaliwa katika zama za Mtume Muhammad (SAW) na akalelewa chini ya malezi ya Mtume (SAW) na baba yake, Amiru al-Mu’minin, Ali ibn Abi Talib (AS). Japokuwa alikuwa bado mtoto, alishuhudia wahyi wa Qur’ani ukiteremka akiwa karibu na Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW).
Baadhi ya aya zinabainisha hadhi tukufu ya Imam Hussein (AS), huku nyingine zikionyesha maana za kiroho na kimaarifa ambazo hujidhihirisha wazi ndani ya maisha ya Imam huyu mtukufu.
1. Aya ya Mahaba (Mawaddah)
"(Muhammad) Sema: ‘Sikuombeni malipo yoyote isipokuwa kuwapenda jamaa zangu wa karibu.’" (Surat Ash-Shura: 23)
Wanazuoni wa Hadith kama Ahmad ibn Hanbal, Ibn Munzir, na wengineo wameripoti kutoka kwa Ibn Abbas kuwa walipoisikia aya hii, Maswahaba walimuuliza Mtume (SAW): “Ni nani hawa jamaa wa karibu ambao tumeamrishwa tuwapende?” Mtume akajibu: "Ali, Fatimah, na wana wao wawili Hassan na Hussein (AS)."
2. Aya ya Utakaso (Tathir)
"Hakika Allah anataka kuwaondolea uchafu watu wa nyumba (Ahlul Bayt) na kuwatakasa kikamilifu."_ (Surat Al-Ahzab: 33)
Kulingana na riwaya nyingi mashuhuri katika vyanzo vya Kishia na Kisunni, “Ahlul-Bayt” wanaotajwa hapa ni Fatimah az-Zahra (SA), Ali (AS), Hassan (AS), na Hussein (AS). Ummu Salama (RA), mke wa Mtume, alishuhudia Mtume (SAW) akimwambia Bibi Fatima (SA): “Mlete mume na watoto wako karibu nami.” Walipokusanyika aliwatia ndani ya shuka (kiswahani) kisha akisoma aya hii ya utakaso juu yao.
3. Aya ya Mubahala
Aya ya Mubahala pia inahusu Hadhi ya Juu ya Imam Hussein (AS)
Katika tukio la kihistoria la Mubahala, Wakristo wa Najran walijadiliana na Mtume Muhammad (SAW) kuhusu ukweli wa Ukristo. Baada ya mjadala mrefu, walikubaliana kwamba kila upande ulete jamaa zake na waombe laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie wale waongo.
Qur’ani Tukufu inasema:
"Na basi yeyote atakayebishana nawe baada ya kujua ukweli, sema: ‘Njooni, tuwaite watoto wetu na watoto wenu, wake zetu na wake zenu, sisi wenyewe na nyinyi wenyewe, kisha tumuombe Mwenyezi Mungu awalani waongo miongoni mwetu. " (Surat Al-Imran: 61)
Riwaya maarufu kutoka madhehebu yote mbili zinasema kuwa Mtume (SAW) aliwaleta tu Ali (AS), Fatimah (SA), Hasan (AS), na Hussein (AS). Neno “watoto wetu” katika aya hii limetafsiriwa kuwa ni Hasan na Hussein (AS).