IQNA

Mtafiti: Ujumbe wa Imamu Hussein (AS) waugusa ubinadamu wote

11:18 - June 30, 2025
Habari ID: 3480875
IQNA – Mwanazuoni na mtafiti wa Kiislamu amesisitiza umuhimu wa kimataifa na wa milele wa harakati ya Imam Hussein (AS), akiuelezea kama ujumbe wa kibinadamu unaowagusa watu wote, bila kujali dini wala asili.

Hujjatul Islam Mahdi Shariat-Tabar alisema, “Ili kufikisha ujumbe wa Ashura kwa kizazi cha leo, ni lazima kwanza tuuelewe kwa kina,” akielekeza katika hotuba, barua, na matendo ya Imamu Hussein (AS) wakati wa tukio la Karbala.

Kwa mujibu wake, maandiko hayo yamejaa “maadili ya kina ya kibinadamu, kiroho, na kijamii.”
Akasema kuwa maadili hayo yanapaswa kuwasilishwa kwa njia inayowavutia vijana wa sasa. “Tunapaswa kutumia lugha ya kisasa, iliyo wazi na inayoendana na mtazamo wa kiakili wa kizazi cha leo,” alifafanua.

Alisisitiza matumizi ya uandishi, mashairi, sanaa za maigizo, vyombo vya kidijitali, na hasa mitandao ya kijamii kama nyenzo bora za kufikisha ujumbe huo.

Kwa mujibu wa Shariat-Tabar, Ashura inawakilisha “uhuru, heshima, imani kwa Mwenyezi Mungu, maadili, uaminifu kwa uongozi wa haki, kupinga dhulma, na kusimama na wanyonge” , maadili alielezea kuwa “yanaheshimiwa na dhamiri yoyote iliyoamka.”

Akanukuu mifano ya kihistoria ya watu wasio Waislamu waliovutiwa na kujitolea kwa Imamu Hussein (AS), wakiwemo akina Mahatma Gandhi.

 “Gandhi mwenyewe alikiri kuwa kusoma kuhusu harakati ya Imamu Hussein (AS) kulimsaidia kugundua njia ya uhuru wa India,” aliongeza.

Pia alielezea wasiwasi wake kuhusu namna harakati ya Karbala inavyoweza kupotoshwa. “Kama alivyosema Shahidi Morteza Motahhari katika kitabu chake Hamaseh Husseini, upotoshaji wa makusudi au usio wa makusudi unaweza kuiondolea Ashura roho yake ya mapinduzi,” alionya. “Kuionesha kama huzuni ya kibinafsi pekee au kuifanya iwe chombo cha maombezi ya kimya kunapotosha maana halisi ya tukio hilo.”

Aliikosoa hali ya ibada ya maombolezo inayozingatia tu ishara kama kupiga vifua, akisema kwamba “desturi hizi zinaweza kukosa maana ya kitamaduni kwa kizazi cha leo na hata kuharibu taswira ya dini.” Alitoa wito wa kugeuza mikusanyiko ya maombolezo kuwa majukwaa ya kufikiri kwa kina na tafakari yenye maana.

Akasema, “Iwapo falsafa ya harakati ya Imamu Hussein (AS) itafafanuliwa kwa uwazi, inaweza kuhamasisha kila binadamu huru, awe Mwislamu au la.”

Akaongeza wito kwa wanazuoni, wasanii, waandishi, na watu wa utamaduni kuendeleza urithi wa Ashura kupitia mbinu za kisasa na ushiriki wa kielimu wa kina.

3493655

Kishikizo: imam hussein as
captcha