IQNA

Imam Hussein (AS) katika Qur’an – Sehemu ya 2

Yale Qur’ani inasema kuhusu dhulma aliyoipata Imam Hussein (AS)

22:02 - July 03, 2025
Habari ID: 3480887
IQNA – Dhulma aliyoipata Imam Hussein (AS) ni ya wazi na ya kina kiasi kwamba inaweza kuchukuliwa kuwa ni taswira halisi ya baadhi ya aya tukufu za Qur’ani.

Alipoinuka Imam Hussein (AS) dhidi ya utawala dhalimu na usio halali wa Yazid bin Muawiya, aliachwa peke yake bila msaada. Hakuna aliyemsaidia, na hatimaye alizingirwa na kuuawa shahidi baada ya vita vya kumwaga damu huko Karbala mnamo mwaka wa 61 Hijri saw ana 680 Miladi.

Hivyo basi, dhulma aliyokumbana nayo Imam Hussein (AS) ni ya wazi mno na ya kusikitisha kiasi kwamba ni mfano dhahiri wa baadhi ya aya za Qur’an Tukufu.

Katika aya moja, Allah (SWT) anasisitiza juu ya utukufu wa uhai wa mwanadamu na kutamka kwamba anayeuawa kwa dhulma, mlinzi wake ana haki ya kutafuta haki:

“Wala msiue nafsi ambayo Mwenyezi Mungu amekataza kuiua isipokuwa kwa haki. Na anayeuawa kwa dhulma, basi tumempa mrithi wake mamlaka [ya kutafuta haki]...”
(Aya ya 33 – Surah Al-Isra)

Heshima ya maisha ya mwanadamu ni kanuni inayopatikana katika dini zote na mifumo ya maadili. Lakini katika mafundisho ya Kiislamu, mfano wa juu kabisa wa kuuliwa kwa dhulma ni kuuliwa kwa Imam Hussein (AS) pamoja na maswahaba wake waaminifu. Katika baadhi ya riwaya, imesemwa kuwa mlinzi wa damu ya Imam Hussein (AS) ni Imam Mahdi Al-Muntadhar (Allah Aharakishe Kudhihiri Kwake), ambaye kwa idhini ya Allah (SWT) atadhihiri siku moja kuusimamisha uadilifu na kulipiza kisasi cha kuuawa Imam Hussein (AS) kwa dhulma.

Aya nyingine ya Qur’an inazungumzia wale waliodhulumiwa na kupewa ruhusa ya kujitetea:

“Wameruhusiwa kupigana wale wanaopigwa kwa sababu wamefanyiwa dhulma. Na kwa yakini Mwenyezi Mungu anao uwezo wa kuwapa ushindi.”
(Aya ya 39 – Surah Al-Hajj)

Kwa mujibu wa baadhi ya wafasiri na wapokezi wa hadithi, aya hii pia inaashiria dhulma aliyopata Imam Hussein (AS), kwani alilazimika kupigana ili kulinda dini ya Mwenyezi Mungu na kusimama dhidi ya dhulma na uonevu.

Zaidi ya hayo, katika kisa cha dhabihu ya Ismail (AS) kilichoelezwa katika Qur’an, Allah alimwamuru Nabii Ibrahim (AS) amchinje kondoo aliyeletwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu badala ya mwanawe. Dhabihu hiyo tukufu imeitwa kuwa ni "dhabihu kuu".

“Na tukamkomboa kwa dhabihu kubwa.”
(Aya ya 107 – Surah As-Saaffaat)

Kwa mujibu wa baadhi ya fasiri za kina, “dhabihu kubwa” haimaanishi tu kondoo, bali inaashiria ukweli mkubwa zaidi. Baadhi ya wafasiri wa Qur’ani wanaamini kuwa inamhusu mmojawapo wa kizazi cha Ibrahim (AS) ambaye damu yake safi ingemwagika kwa ajili ya Mwenyezi Mungu – naye si mwingine bali ni Imam Hussein (AS). Katika riwaya kutoka kwa Mtume Muhammad (SAW), inasemekana kuwa Mwenyezi Mungu alimfunulia Nabii Ibrahim (AS) habari za kuuawa shahidi kwa Imam Hussein (AS), na Nabii Ibrahim (AS) akalia sana kwa huzuni na uchungu.

3493685

captcha