IQNA

Rambi rambi za Ayatullah Sistani kufuatia moto wa jumba la biashara Iraq ambapo wengi walipoteza maisha

18:39 - July 18, 2025
Habari ID: 3480962
IQNA – Ayatullah Mkuu Sayyid Ali al-Sistani, kiongozi wa juu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Iraq, ametuma salamu za rambi rambi kwa familia za wahanga wa tukio la moto mkubwa uliotokea katika jumba la biashara mjini Kut.

Kwa mujibu wa Al-Kafeel, kiongozi huyo wa Kiislamu alitoa taarifa rasmi ya kutoa pole kwa familia za waliopoteza wapendwa wao.

Katika ujumbe wake, Ayatullah Sistani alimuomba Mwenyezi Mungu awarehemu waliopoteza maisha, awape subira waliopoteza jamaa zao, na awape afueni ya haraka waliojeruhiwa.

Taarifa hiyo ilisoma hivi:
"Tunawapa pole za dhati na rambirambi za kutoka moyoni kwa wote waliopatwa na msiba huu wa kuwapoteza wapendwa wao. Tunamuomba Allah Mtukufu awafunike mashahidi hawa watukufu kwa rehma Zake pana, awape familia zao subira na faraja, na awaponye haraka walioumia."

Takriban watu 77 wamethibitishwa kufariki dunia huku wengine kadhaa wakiendelea kutafutwa, kufuatia moto mkubwa uliozuka usiku na kuiteketeza jengo la ghorofa tano la biashara la Corniche Hypermarket, katika mji wa Kut, mkoani Wasit, mashariki mwa Iraq.

Moto huo ulizuka usiku wa kuamkia Alhamisi na kuwateka ndani wateja na wafanyakazi. Vikosi vya uokoaji vilifanya kazi usiku kucha kuuzima moto na kuwaokoa manusura. Watu 45 waliokolewa salama, baadhi yao wakitoroka kupitia dari kwa msaada wa vikosi vya dharura.

Gavana wa Mkoa wa Wasit, Mohammed al-Mayahi, alielezea tukio hilo kuwa ni "janga na msiba mkubwa," akibainisha kuwa juhudi za uokoaji na uokozi bado zinaendelea.

Afisa wa afya aliyezungumza na shirika la habari la Reuters alisema majina ya watu 59 waliotambuliwa tayari yameandaliwa kwa maziko, lakini miili mingine itahitaji vipimo vya vinasaba (DNA) kutokana na hali mbaya ya maiti hizo.

Maafisa wa jiji walisema vikosi vya dharura vinaendelea kuondoa vifusi ili kupata miili iliyokwama chini.

Shuhuda mmoja, ambaye anaishi karibu na jumba hilo la biashara, alieleza hali ya kutisha:
“Moto ulienea kwa kasi na kuwazuia watu wengi kutoka ndani ya jumba. Kila mtu alikuwa akihangaika kutafuta njia ya kutokea. Niliona miili ya watoto na wanawake ikiwa imeteketea. Ilikuwa ni hali ya kutisha sana,” alisema kwa masikitiko.

Katika tukio jingine tofauti, watu wanne walifariki dunia katika mji wa Karbala, Iraq, baada ya moto na mlipuko uliofuatia katika maghala ya nguo. Inasemekana kuwa mlipuko huo ulitokana na milipuko ya mizinga ya mafuta iliyoathirika na moto huo.

3493885

Kishikizo: iraq Ayatullah Sistani
captcha