Arbaeen ni miongoni mwa mikusanyiko mikubwa zaidi ya kidini duniani, ambapo katika miaka ya karibuni zaidi ya waumini milioni 21 wamekusanyika Karbala, Iraq. Kila mwaka, waumini, hasa Waislamu wa madhehebu ya Shia, husafiri kwa miguu karibu kilomita 80 kutoka Najaf hadi Karbala kwa siku kadhaa, wakikumbuka kuuawa shahidi kwa Imam Hussein (AS) na kukamilika kwa kipindi cha maombolezo cha siku 40. Njiani, wahisani hutoa chakula, malazi na huduma za matibabu bila malipo, wakiakisi moyo wa ukarimu na mshikamano.
Ayatoullah Sistani amesisitiza umuhimu wa swala, akisema, “Inafaa kwa muumini kudumu kuswali katika wakati wake ulioamriwa; kwani mja mpenzi zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule anayejibu kwa haraka zaidi adhana (mwito wa swala) .”
Amebainisha kuwa Ahlul-Bayt (AS) wameonya kuwa “Shifaa’ yao hauitamfikia yule anayebeza swala.”
Akinukuu simulizi kutoka Karbala, Ayatullah Sistani alikumbusha kuwa hata katika uwanja wa vita, Imam Hussein (AS) alimpongeza aliyemkumbusha muda wa swala, akisema, “Umenikumbusha swala. Mwenyezi Mungu akufanye miongoni mwa waja wakumbukao,” kisha akasimama kuswali huku mvua ya mishale ikinyesha.
Kiongozi huyo wa kidini nchini Iraq amewahimiza wafanyaziyara kudumisha ikhlasi katika kila tendo, akisisitiza kuwa ni yale tu yanayofanywa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu pekee ndiyo yanayokubaliwa.
Aidha, ametoa msisitizo wa kuvaa na kuishi kwa staha, hasa kwa wafanyaziyara wanawake. Ameukumbusha umma kuwa hata katika mitihani mikubwa ya Karbala, familia ya Mtume ilidumisha mavazi yenye heshima.
Ameonya dhidi ya mavazi yanayobana, mazungumzo yasiyo ya lazima baina ya wanaume na wanawake, na mapambo yasiyo na haja, akihimiza kwamba heshima na utukufu wa Arbaeen viinuliwe kupitia kiwango cha juu cha haya na adabu.
3494214