IQNA

Msimu Mpya wa Mashindano ya Qur'ani ya “Dawlat al-Tilawa” Misri kuanza Novemba

11:53 - January 08, 2026
Habari ID: 3481784
IQNA – Msimamizi mkuu wa mashindano ya vipaji vya Qur’ani nchini Misri, maarufu kwa jina “Dawlat al-Tilawa”, ametangaza kuwa msimu mpya wa kipindi hicho kitaanza rasmi Novemba 2026.

Ahmed Fayeq alisema watazamaji daima huvutiwa na vipindi vyenye maudhui yenye maana na kina, na akasisitiza kuwa mafanikio ya msimu wa kwanza yamezidi matarajio ya waandaaji.

Kwa mujibu wa Fayeq, muda maalum wa kurusha kipindi umewekwa, na kuanzia sasa msimu mpya utakuwa ukitangazwa kila Novemba. Alifafanua kuwa maandalizi ya kipindi yalichukua takribani mwaka mmoja na nusu, na mashindano yalianza kwa ushiriki wa takribani washiriki 14,000 kutoka pembe zote za Misri.

Uhakiki wa usomaji ulifanywa na jopo la majaji lililoteuliwa na Waziri wa Awqaf wa Misri, kwa usimamizi maalum wa wanazuoni wakuu wa Al-Azhar. Hatimaye, watu 300 walichaguliwa kuingia hatua ya pili, na baada ya mashindano makali ya siku tatu mfululizo katika Chuo cha Kimataifa cha Awqaf cha Misri, washiriki 32 pekee walibaki kuingia fainali.

Fayeq aliongeza kuwa idadi ya watazamaji imevuka mamilioni, na sasa timu ya kipindi inafanya kazi kuandaa mbinu mpya itakayodumisha mafanikio ya msimu wa kwanza huku ikileta mshangao na ubunifu katika msimu wa pili.

Alihitimisha kwa kusema kuwa timu ya kipindi inashirikiana kwa karibu na Wizara ya Awqaf, ambayo ilitoa nyenzo zote zilizowezesha mafanikio ya msimu wa kwanza, na sasa maandalizi ya kina yanaendelea kwa njia mbalimbali.

Msimu wa kwanza wa Dawlat al-Tilawa ulitayarishwa kwa ushirikiano na Wizara ya Awqaf na Kampuni ya United Media Services nchini Misri, ukiwa na lengo la kubaini vipaji na wasomaji bora wa Qur’ani kutoka mikoa mbalimbali.

Kipindi hurushwa kupitia vituo vya satelaiti Al-Hayat, CBC, Al-Nas, Misr al-Qur’an al-Karim, pamoja na jukwaa la mtandaoni Watch It, saa tatu usiku kila Ijumaa na Jumamosi.

Jumla ya zawadi za mashindano ni pauni za Kimasri milioni 3.5. Washindi wa kwanza katika makundi ya usomaji na tajwid watapokea pauni milioni moja kila mmoja, na Qur’ani nzima itarekodiwa kwa sauti zao na kurushwa kupitia kituo cha Misr Qur’an Karim. Aidha, watapewa heshima ya kuongoza swala za Taraweeh katika Msikiti wa Hussein wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Kipindi hiki kinajivunia jopo la majaji mashuhuri kutoka ulimwengu wa Kiislamu, akiwemo Hassan Abdel-Nabi, Taha Abdel-Wahab, Mostafa Hosny, na Taha al-Nuamani. Wageni maalum ni pamoja na Osama al-Azhari, Nazir Mohamed Ayyad, Ali Gomaa, Ahmed Nuaina, Abdel-Fattah al-Tarouti, Jaber al-Baghdadi, mwanazuoni wa Uingereza Muhammad Ayoub Asif, na Omar al-Qazabri kutoka Morocco.

3496007

Habari zinazohusiana
captcha