Katika maandamano hayo, waandamanaji walichoma bendera za utawala haramu wa Israel na kutaka kufutwa kwa makubaliano ya kuwa na uhusiano kati ya Morocco na utawala huo katili, huku wakitangaza kuunga mkono mapambano ya Wapalestina ya kupigania ukombozi hasa mapambano ya sasa ya wakazi wa Gaza.
Wanaharakati wa “Harakati ya Kitaifa ya Kivitendo ya Kutetea Palestina,” shirika lisilo la kiserikali, waliandaa maandamano hayo mbele ya jengo la bunge mjini Rabat kama ishara ya mshikamano na upinzani wa Wapalestina dhidi ya mashambulizi ya Israel na kulaani jinai za jeshi la Israel katika Ukanda wa Gaza.

Washiriki walipeperusha bendera za Palestina na kubeba mabango yenye ujumbe wa kuunga mkono wananchi wa Palestina, yakiwemo maandishi yanayowasalimu Wapalestina na kukumbuka ushindi wa kihistoria wa Kimbunga cha Al-Aqsa dhidi ya wavamizi Wazayuni na madola ya kibeberu yanayowaunga mkono.
Mabango mengine yalilaani mauaji ya halaiki, njaa ya kimfumo na mzingiro wa Gaza, yakiyataja kama uhalifu wa Kizayuni unaofanana na wa Wanazi, unaotekelezwa kwa ushirikiano wa baadhi ya nchi za Kiarabu na Magharibi.
Pia kulikuwa na ujumbe unaosema kuwa na uhusiano na Israel ni sawa na kushiriki katika mauaji ya wakazi wa kambi za Gaza, na kwamba watu wa Morocco, wakiwa wamoja na Umma wa Kiislamu, wanasimama dhidi ya uchokozi na pamoja na mapambano hadi ukombozi wa Palestina.
Waandamanaji walipaza kauli mbalimbali kama “Gaza ni alama ya heshima,” “Licha ya njaa na uharibifu, Gaza ni huru na haitasalimu,” na “Enyi watu huru popote mlipo, simamisheni mauaji na fungulieni njia za kupitisha misaada.”
Kauli nyingine zililaani uharibifu unaoendelea Gaza, kuutaja utawala wa Kizayuni kuwa waoga na wauaji wa watoto, na kutaka kundi hilo kufikishwa kwenye mahakama ya umma. Maandamano hayo yaliishia kwa kuchomwa kwa bendera ya Israel.
Morocco imeendelea kushuhudia maandamano makubwa ya mara kwa mara na shughuli za mshikamano na Wapalestina licha ya serikali yake kuendeleza mchakato wa kuwa na uhusiano na utawala wa Israel. Wananchi wengi wa Morocco wanataka makubaliano hayo yafutwe. Israel, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Bahrain walisaini makubaliano ya usnormalishaji tarehe 15 Septemba 2020, yanayojulikana kama Mapatano ya Abraham, na baadaye Morocco na Sudan pia zilijiunga na makubaliano hayo.
3496024