Maandamano hayo makubwa yamekuwa yakifanyika kila wiki tangu Oktoba mwaka jana, wakati utawala wa Israel ulipoanzisha mashambulizi yake ya kikatili dhidi ya Ukanda wa Gaza unaozingirwa. Uvamizi huo wa Israel hadi sasa umepelekea kuuawa shahidi karibu Wapalestina 41,000 wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto.
Waandamanaji siku ya Ijumaa "wamelaani jinai zinazoendelea za adui wa Kizayuni ikiwa ni Pamoja na kuuvunjia heshima Msikiti wa Al-Aqsa, na askari wa Kizayuni kurarua nakala za Qur'ani Tukufu, katika msikiti wa Ukanda wa Gaza.”
Washiriki "walisisitiza kuwa adui Muisraeli huvuka mistari yote myekundu na kukiuka kanuni na sheria zote za kimataifa," iliongeza.
Maandamano hayo yanajiri huku picha zilizotolewa Ijumaa iliyopita zikiwaonyesha wanajeshi waovu wa utawala haramu wa Israel wakizidharau nakala za Qur'ani Tukufu katika msikiti mmoja katika Ukanda wa Gaza unaozingirwa.
Kituo cha habari cha Qatar cha Al Jazeera kimesema kimepata picha hizo kutoka kwenye video iliyochukuliwa na wanajeshi wa Israel na ndege zisizo na rubani ambazo zilipatikana Gaza. Picha hizo zilionyesha wanajeshi wa Israel wakivamia Msikiti wa Bani Saleh ulioko kaskazini mwa Ukanda wa Gaza na kisha kurarua na kuchoma nakala za Qur’ani ndani ya msikiti huo.
Waandamanaji wa Yemen pia walikashifu "serikali vibaraka za Kiarabu" na ukimya wa mataifa ya Kiislamu juu ya kitendo cha wanajeshi wa Israel cha kuvunjia heshima Qur'ani, uvamizi wa mara kwa mara katika Msikiti wa Al-Aqsa, na kauli ya uchochezi ya Israel kuhusu kujenga sinagogi katika msikiti huo ambao ni eneo la tatu la Uislamu takatifu.
Waandamanaji wa Yemen wamesisitiza uungaji mkono wao unaoendelea kwa watu wa Palestina na juhudi zao za muqawama , yaani mapambano ya kupigania ukombozi. Wameeleza uungaji mkono kamili kwa hatua za kukabiliana na jinai zinazofanywa na adui Mzayuni na kusisitiza utayarifu wao wa kukabiliana na uvamizi unaotelekezwa Marekani na Israel, pamoja na njama zozote zinazolenga taifa la Palestina na maeneo yake matakatifu.
3489710