IQNA

Algeria yakosoa hatua ya Morocco kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni

21:51 - December 12, 2020
Habari ID: 3473450
TEHRAN (IQNA)- Waziri Mkuu wa Algeria amekosoa hatua ya Morocco kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Akizungumza Jumamosi, Waziri Mkuu wa Algeria, Abdelaziz Djerad, amesema Waalgeria wataungana kukabiliana na ajinabi ambao wanawafikisha Wazayuni katika mipaka yao.

Katika hotuba kwa mnasaba wa maadhimisho ya mwaka wa 60 wa uhuru wa Algeria kutoka mkoloni Mfaransa, Djerad amesema: “Algeria inalengwa na na njama na hivyo Waalgeria wanapaswa kushirikiana kutatua matatuzo ya nchi yao.

Aidha amesema Waalgeria wanapaswa kudumisha uthabiti katika nchi yao na wakabiliana na ajinabi ambao wanataka kuufikisha utawala wa Kizayuni katika mipaka ya Algeria.

Juzi Alhamisi, Mfalme wa Morocco Mohammed VI alimwarifu Rais Donald Trump wa Marekani kwenye mazungumzo kwa njia ya simu kuwa amekubali kurejesha mawasiliano ya kiserikali na kuanzisha uhusiano wa kibalozi na utawala wa Israel haraka iwezekanavyo.

Marekani nayo imesema itatambua mamlaka ya Morocco katika eneo la Sahara Magharibi la nchi hiyo ambalo limejitangazia uhuru. Ufalme wa Morocco umetangaza kuwa Marekani hivi karibuni itafungua ubalozi mdogo huko Sahara Magharibi.

Uamuzi huo wa Morocco kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel unafuatia uamuazi sawa na huo uliochukuliwa miezi ya karibuni na Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain na Sudan. Nchi zingine za Kiarabu ambazo zina uhusiano rasmi na utawala bandia wa Israel ni Misri na Jordan.

3940639

captcha