
Ubunifu huu wa Malaysia umeashiria hatua muhimu katika elimu ya Qur'ani kwa wanafunzi wenye ulemavu wa macho, kwa kuwaongezea upatikanaji wa maarifa ya dini na pia masomo mengine.
Waziri wa Masuala ya Dini wa Malaysia, Zulkifli Hasan, alisema kifaa hicho, kilichobuniwa na kampuni ya Edote Sdn Bhd, kimeweza kutatua changamoto kubwa zilizokuwa zikiwakabili walimu wasioona, ambao hapo awali walitegemea Misahafu ya maandishi ya nukta nundu (Braille) ya kawaida ambayo ni mizito na mikubwa kubeba.
Alisema ubunifu huo ni “matokeo ya utafiti wa Wamalaysia wenyewe, unaotoa suluhisho nafuu zaidi na la kisasa,” akiongeza kuwa ni hatua inayostahili pongezi. Alifafanua kuwa hapo awali, watu wenye ulemavu wa macho walilazimika kutumia nakala ya Qur'ani ya nukta nundu yenye juzuu sita na uzito wa takribani kilo 10, ilhali sasa wanahitaji tu kifaa cha eBraille chenye uzito usiozidi kilo moja.
Kauli hizo alizitoa baada ya kufungua Warsha ya Matumizi ya Kifaa cha eBraille pamoja na hafla ya kukabidhi vifaa hivyo kwa walimu wa Qur'ani wenye ulemavu wa macho, iliyofanyika Alhamisi mjini Kuala Lumpur. Tukio hilo liliandaliwa kwa ushirikiano kati ya Yayasan Dakwah Islamiah Malaysia (YADIM), Baraza la Dini la Kiislamu la Maeneo ya Shirikisho (MAIWP) na Edote Sdn Bhd.
Kwa mujibu wa Zulkifli, jumla ya vifaa 10 vya eBraille vilisambazwa siku hiyo, ambapo viwili kati ya hivyo viliwekwa katika Msikiti wa Tuanku Mizan Zainal Abidin huko Putrajaya na Msikiti wa Sultan Abdul Samad Jamek ili kuendeleza masomo yanayotumia teknolojia hiyo. Alisema lengo ni kuwafunza walimu zaidi wa Qur'ani wanaoweza kutumia kifaa hicho kwa ufasaha, ili watoto wenye ulemavu wa macho wapate fursa bora zaidi ya elimu ya dini, hususan Qur'ani.
Kwa upande wake, Rais wa YADIM, Datuk Dr Hasan Bahrom, alisema katika hotuba yake kuwa jumla ya walimu 20 wa Qur'ani wenye ulemavu wa macho, wakiwa na wasaidizi wao, walishiriki katika warsha hiyo iliyolenga kuimarisha mbinu za ufundishaji wa Qur'ani kupitia matumizi ya teknolojia ya kisasa. Ili kuhakikisha mafanikio ya mpango huo, alisema kiasi cha RM90,000 kimetolewa na wizara ya masuala ya dini, sambamba na wito wa Waziri Mkuu Anwar Ibrahim kwa taasisi za serikali kutumia teknolojia kikamilifu katika kuhudumia wananchi.
Aliongeza kuwa mpango huo unaendana na Mpango Kazi wa Taasisi za Kidini kwa Waislamu Wenye Ulemavu 2024–2028, unaosisitiza elimu ya dini na haki za watu wenye ulemavu katika kutekeleza ibada zao kama Waislamu. Alisema YADIM itaendelea kupanua, kufuatilia na kuboresha programu kama hizi kupitia ushirikiano na vyombo vya habari, mashirika yasiyo ya kiserikali na sekta binafsi, kwa matumaini kwamba juhudi hizi zitawawezesha watu wenye ulemavu ndani ya ajenda pana ya maendeleo nchini humo.
3496013