IQNA

Al‑Saif awa Mshia wa kwanza kuteuliwa kuwa waziri katika Baraza la Mawaziri la Saudia

14:55 - February 15, 2026
Habari ID: 3481937
IQNA – Mfalme Salman bin Abdulaziz wa Saudi Arabia amemteua kiongozi mmoja kutoka jamii ya Waislamu wa madhehebu ya Shia kuwa Waziri wa Uwekezaji wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa mtandao wa Al‑Hadath, Fahd bin Abduljalil bin Ali Al‑Saif amekuwa Mshia wa kwanza kushika wadhifa wa waziri ambapo amepewa wadhifa muhimu kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Uwekezaji katika Baraza la Mawaziri la Saudi Arabia. Kabla yake, nafasi hiyo ilikuwa ikishikiliwa na Khaled Al‑Falih.

Uteuzi wa Al‑Saif unakuja kufuatia mabadiliko ya kiutawala, baada ya mtangulizi wake kutoa kauli za ukosoaji kuhusu mradi mkubwa wa “The Line”.

Al‑Saif alizaliwa mwaka 1976 katika Mkoa wa Sharqiya, na ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha King Fahd cha Petroli na Madini. Ana zaidi ya miaka ishirini ya uzoefu katika nyanja za usimamizi wa madeni, uwekezaji, na ufadhili wa kimataifa. Tangu mwaka 2021, amekuwa akisimamia maeneo muhimu ya ufadhili wa kimataifa na mikakati ya uwekezaji katika Mfuko wa Uwekezaji wa Umma wa Saudi Arabia (PIF).

Pia ni mwanzilishi wa Ofisi ya Usimamizi wa Deni la Umma katika Wizara ya Fedha, na amekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa kwanza wa Kituo cha Kitaifa cha Usimamizi wa Madeni. Aidha, ana uzoefu wa juu wa kiutawala katika benki za SABB na HSBC Saudi Arabia.

Al‑Saif amehudumu pia kama mjumbe na mwenyekiti wa bodi katika taasisi kadhaa muhimu, zikiwemo NEOM, ACWA Power, Gulf International Bank, King Abdullah Economic City, Kampuni ya Maendeleo ya Uwanja wa Ndege wa King Salman, pamoja na Taasis ya Future Investment Initiative.

Miongoni mwa mafanikio yake muhimu ni kuanzisha mfumo wa ufadhili wa kijani (green financing), kutoa kwa mara ya kwanza hati fungani za kijani za miaka 100 kupitia mfuko wa taifa wa uwekezaji, na kuongoza programu za kutofautisha vyanzo vya ufadhili kwa miradi mikubwa ya kimkakati.

3496418

Kishikizo: shia saudi arabia
captcha