IQNA

Imam Khamenei: Ubunifu utumike kukabiliana na hujuma ya kiutamaduni

8:24 - December 11, 2013
Habari ID: 1337090
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuhusu wajibu wa kuwepo jitihada zenye ubunifu katika kukabiliana na hujuma ya kiutamaduni.

Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo Jumanne katika kikao chake na mkuu na wajumbe wa Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni. Kiongozi Muadhamu ameashiria harakati za mamia ya vyombo vya habari vya sauti, taswira, maandishi na Intaneti kote duniani ambavyo vinalenga kuathiri vibaya fikra na tabia za wananchi wa Iran na kusema kuwa, kunahitajika jitihada zenye ubunifu na zenye hekima ili kukabiliana na hujuma hizo za kiutamaduni. Katika nasaha zake kwa Wizara ya Utamaduni na Muongozo wa Kiislamu pamoja na Shirika la Utangazaji la Iran kuhusu kukabiliana na hujuma za kiutamaduni, Kiongozi Muadhamu amesisitisza kuwa: ‘Kazi zinazopaswa kupewa kipaumbele ni pamoja na kutarjumu vitabu vyenye manufaa, kutengeneza filamu za kuvutia kwa kutegemea uwezo mkubwa wa kutengeneza filamu, kutengeneza michezo ya kompyuta yenye manufaa, kuhimiza michezo yenye msisimko na kutengeneza wanasesere wa kuvutia na wenye maana.’

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuna udharura wa kutambua kikamilifu matukio mapya ya mashambulizi ya kiutamaduni kabla hayajajipenyeza Iran. Amesema kukaa tu na kusubiri kujihami wakati wa hujuma ya utamaduni ndio hali mbaya na yenye hasara zaidi katika kukabiliana na suala hilo. Ayatullahil Udhma Khamenei pia amesisitiza kuhusu wajibu wa kuzingatiwa kikamilifu udharura wa kuendeleza ustawi wa kielimu katika vyuo vikuu na taasisi za utafiti. Amesema hivi sasa, kuna wimbi la ‘sisi tunaweza’ miongoni mwa vijana wa Iran na kwamba wimbi hilo linapaswa kutumiwa ili kuifikisha Iran katika kilele cha ubora wa kisayansi na kuwa marejeo ya kisayansi sambamba na kufikiwa ustaarabu mpya wa Kiislamu. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameelezea wasi wasi wake kuhusu kutozingatiwa ipasavyo lugha ya Kifarsi na hujuma dhidi ya lugha hiyo. Amesema Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni linapaswa kukabiliana na udhoofishaji lugha maridadi na yenye kina kirefu ya Kifarsi sambamba na kueneza na kuimarisha lugha hii katika nyanja zote. Kiongozi Muadhamu amesema, kuandikwa msingi wa kielimu na kifalsafa katika mabadiliko ya Sayansi za Jamii ni moja ya hatua za kimsingi zinazopaswa kuchukuliwa na baraza hilo. Aidha ametaka kuwepo juhudi za kutafuta njia za kukabiliana na masuala kama vile talaka, ufisadi wa kifedha na uhalifu.

1337043

captcha